VIGOGO
mashuhuri wa Chadema waliowahi kuwa mawaziri wakuu; Edward Lowassa na
Frederick Sumaye, jana waligeuka gumzo ndani ya Mkutano Mkuu Maalumu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kumchagua Rais John Magufuli, kuwa
Mwenyekiti wa tano wa chama hicho.
Gumzo
hilo, lilianzishwa na Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba,
alimpomtaka Askofu wa Kanisa la Ufufuko na Uzima, Josephat Gwajima,
asimpotoshe Magufuli ili yasije yakampata ya Sumaye, ambaye sasa
anachezea mchangani Kibaha.
Sumaye mchangani
“Hata akina Sumaye hawakuunda vyama vyao. Bado wanahangaika; na sasa Sumaye anacheza mchangani Kibaha,” alisema Makamba.
Sumaye
ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na NEC ya CCM, kwa sasa
anawania uongozi wa Kanda ya Pwani katika Chadema. Kabla ya kusema kuwa
Sumaye anahangaika na siasa za mchangani, Makamba alimtaka Gwajima
kuacha uongo na kusingizia viongozi wa CCM.
Makamba
aliyepewa nafasi ya kumuombea kura Rais John Magufuli kwa wajumbe wa
Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, alisema anamtia moyo Magufuli asiogope
kuongoza chama, kwani hataongoza peke yake bali wapo wanachama wengi
watakaomsaidia kazi hiyo.
“Wewe siyo wa kwanza kukataa kazi hii. Hata watangulizi wako Kikwete na Benjamin Mkapa nao walifanya hivyo hivyo,“ alisema Makamba ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Makamba
alisema hata manabii na mitume wengi, kama Haruni, Mussa, Yona au Yunus
na Yeremia walifanya vivyo hivyo, walipopewa utume au unabii na Mungu,
kwani waliogopa kufanya kazi hizo lakini, alisema mara zote Mungu
aliwaagiza kuwa wasiogope kuwa manabii na mitume, kwani atatia maneno
kwenye vinywa vyao.
Aidha,
Makamba alitaka viongozi wa dini mfano Askofu Gwajima, waache kumfitini
Kikwete eti kwamba alikuwa hataki kumpa uenyekiti Magufuli.
“Askofu
Gwajima alikuwa anasingizia kuwa Jakaya kiongozi wetu mpendwa hataki
kukupa uenyekiti. Alikuwa akikuhimiza kuwa kama hataki uunde chama
chako. Huu ni uongo. Gwajima amemaliza uongo wote,” alisema Makamba na kumuomba Magufuli asisikilize uongo wa kiongozi huyo wa kiroho.
Makamba
alimtaka Askofu Gwajima atambue kuwa hata baadhi ya wana-CCM
waliojiengua mwaka jana, hawakuunda vyama vyao badala yake wameangukia
pua.
Aliwataka
wajumbe wa mkutano huo, kumpa kura zote za ‘Ndiyo’ Rais Magufuli, kisha
Makamba akaanza kutumia uhodari wake wa misemo, methali, mafumbo na aya
za Biblia na Kurani Tukufu.
“Mzigo
wa chama ulikuwa umebebwa na Mkwere Kikwete ambaye sasa anaondoka; na
kwa kuwa kuna msemo kuwa ‘mzigo mzito mpe Mnyamwezi au Msukuma, nawaomba
wajumbe wote sasa mzigo wa chama tumpe Msukuma Magufuli,” alisema na kauli yake hiyo ilishangiliwa na wajumbe.
Lowassa na ufisadi
Akielezea
aina ya kiongozi anayetoka CCM na anayeingia, Makamba alisema kuwa
anayetoka, Kikwete ni mpiganaji wa ufisadi, kwa kuwa alifikia hatua ya
kumtosa rafiki yake Edward Lowassa, kuwa hafai kuwa Rais kwa kuwa
anatuhumiwa kwa ufisadi.
Alisema
kada wa chama hicho anayeingia baada ya Kikwete, Dk Magufuli yeye ndiye
muasisi wa Mahakama ya Mafisadi, ambayo tayari imeshaanzishwa kwa
Sheria ya Bunge. Kwa mujibu wa Makamba, Kikwete ni kiongozi aliyepiga
vita umasikini na anapoondoka, anayeingia Dk Magufuli msimamo wake ni
asiyefanya kazi na asile.
Kumchinja Kobe
Naye
mmoja wa vigogo wa Chadema aliyerejea CCM, Fred Mpendazoe, alikuja na
dhana ya namna ya kumchinja kobe, akifananisha na utaratibu uliotumika,
kukata jina la Lowassa katika majina 38 ya wagombea urais.
Mpendazoe
alisema Kikwete alifanya ‘timing’ sana kushughulikia ufisadi ndani ya
chama hicho, kwa kuwa kati ya makada hao 38 waliokuwa wakiwania urais,
baadhi akiwemo Lowassa walikuwa na tuhuma za ufisadi na kukatwa kwa
majina yao, kulifanyika kwa wakati sahihi.
Kuachana na nzi
Mpendazoe
pia alisema Wasambaa walimfundisha msemo mmoja kwamba, mtu akitaka
asifuatwe na nzi, anatakiwa atupe mzoga na kuongeza kuwa, hatua ya
wagombea wenye tuhuma za rushwa kutupwa, CCM ilitupa kibudu.
Kwa
mujibu wa Mpendazoe, kuhamia Chadema kwa Lowassa, kulisababisha chama
hicho na Ukawa waliomuunga mkono, kupoteza ajenda, kwa kuwa walimpokea
mtu waliyezunguka nchi nzima wakimtuhumu kwa ufisadi tena wakisema wanao
ushahidi.
“Walipompokea Lowassa, nikasema basi mchezo umekwisha wamepoteza ajenda,” alisema Mpendazoe huku akishangaa kitendo cha Ukawa kudai demokrasia imekuwa ikibanwa.
Gia angani
Mpendazoe
alisema anashangaa kusikia Magufuli anabana demokrasia na kuhoji kati
ya chama kilichotangaza nafasi ya urais na kuruhusu wagombea 38
kugombea, huku mchujo ukifanyika hadharani na kilichompata mgombea
kwenye chopa (helikopta), ni kipi chenye demokrasia?
Akifafanua
zaidi, Mpendazoe alisema Chadema ilimpata mgombea wake angani ndani ya
helikopta, na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe alipokwenda katika vikao,
akasema chama hicho kimebadilisha gia angani.
“Nilihoji
iweje uamuzi huo ufanyike bila vikao,” alisema na kuongeza kuwa
kilichofanyika kilikuwa sawa na biashara na kuhoji kwa nini chama hicho
kisisajiliwe Brela (Ofisi ya Msajili wa Makampuni) ili kufanya biashara.
CCM B
Naye
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alihoji yeye kuitwa CCM B, baada ya
Rais Magufuli kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole na kusema
inakuwaje yeye aliyetoka katika chama hicho mwaka 1995, apewe jina hilo.
Alisema
kama kupewa cheo na Magufuli, ndio sababu ya kuitwa CCM B, basi hata
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi
na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, ni CCM B kwa kuwa aliteuliwa kuwa Mbunge
na Rais Jakaya Kikwete.
Mrema
alisema kama kuitwa kwake CCM B ni kutokana na kutoka ndani ya CCM;
basi Lowassa na Sumaye ni CCM A, kwa kuwa wao wametoka mwaka jana wakati
yeye ametoka tangu 1995.
Haeleweki
Naye
Magufuli alisema alimshangaa Rais mstaafu Benjamini Mkapa, kwa kumteua
mtu mmoja kuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo, wakati waliofanyakazi
na Waziri Mkuu huyo, akiwamo yeye waliona kuwa ni mtu asiyeeleweka.
Waziri Mkuu wa Mkapa, alikuwa Frederick Sumaye.
Kauli
hiyo ya Magufuli, ilitanguliwa na ya Kikwete, ambaye alishangaa kuona
mtu aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, sasa anagombea uenyekiti wa Kanda.