MTUHUMIWA wa ujambazi Msafiri Suleiman maarufu kama Juma Msukuma ameuawa wakati akijaribu kuwatoroka Polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Julai 28 mwaka huu majira ya saa 10.30 jioni katika eneo la Igoma kata ya Igoma jijini Mwanza.
Kamanda Msangi alisema mtuhumiwa siku hiyo alikuwa amekamatwa na Polisi akituhumiwa kufanya matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha akishirikiana na wenzake watatu.
Aliwataja watu hao aliokuwa akishirikiana nao ambao kwa sasa wamekamatwa na polisi kuwa ni Jackson Magesa ( Nyakibimbi), Samwel Mwita na Boniphace Nyamhanga.
Kamanda alisema baada ya mahojiano na polisi mtuhumiwa alikiri kuhusika na uhalifu na akakubali kwenda kuwaonesha askari sehemu aliyoficha silaha maeneo ya Buhongwa mlimani.
Alisema walipofika eneo husika aliwaonesha mkasi mkubwa wa kukatia vyuma na kipande cha nondo, huku akiwathibitishia kuwa silaha alikuwa ameichimbia ardhini katika eneo hilo.
“Wakati askari wakiwa kwenye harakati za kufukua ili waichukue silaha hiyo, mtuhumiwa alitumia mwanya huo kuanza kukimbia huku akiwa na pingu mkononi, askari walifyatua hewani risasi tatu, lakini mtuhumiwa hakutii amri hiyo ndipo alipopigwa risasi mguuni na kufanikiwa kukamatwa”, alifafanua.
Alisema alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.
“ Watuhumiwa aliokuwa akishirikiana nao tumewakamata na tumewakuta wakiwa na bunduki aina ya Rifle Mark 4 ikiwa na risasi nne, ikiwa na kitako cha bunduki waliyopora, nyundo moja na vipande vitatu vya nondo”, alisema.
“ Watuhumiwa hao tunawashikilia kwa matukio ya unyang’anyi Nyashishi, Buhongwa, Bulale, Nyambichi na Mwananchi ambapo walipora silaha toka kwa mlinzi wa Kampuni ya Paroma Patrol Security Service”, aliongeza