Mmoja wa waandishi mahiri wa habari za uchunguzi jijini Dar es salaaam,ametekwa na wanawake wachuuzi wa biashara haramu ya kuuza miili almaarufu kama machangudoa au madadapoa jijini Dar es salaam.
NI KWENYE OPARASHENI MAALUM
Tukio la kutekwa kwa mwanahabari wetu, lilijiri usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita jirani na gesti maarufu iliyopo maeneo ya Sinza-Mori jijini hapa, ikiwa ni siku ya tatu tangu alipozama kwenye oparesheni maalum ya kuchunguza uwepo wa biashara hiyo tangu ilipopigwa marufuku na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
KABLA YA OPARESHENI
Kabla ya kujichimbia kwenye oparesheni hiyo akijifanya changudoa mzoefu, mapema wiki hii, OFM ilipokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya Sinza wakisema kuwa, madadapoa hao wanaendelea kutikisa eneo hilo kwa kuuza miili yao licha ya kupigwa marufuku na Makonda, wakijigamba kwamba mkuu wa mkoa hawawezi.
TIMU KAZI YAUNDWA
Baada ya kupokea malalamiko hayo, Kamanda Mkuu wa OFM alipanga timu kutoka kitengo hicho, kwa kumuandaa ‘changudoa’ na wapigapicha ili kwenda kujua tatizo liko wapi hasa mpaka akina dada hao washindwe kuachana na biashara hiyo haramu licha ya serikali kutoa matamko kadhaa ya kuwapiga marufuku.
SIKU YA KWANZA MZIGONI
Siku ya kwanza ya ‘kujiuza’, ilikuwa Jumatatu iliyopita ambapo mwandishi wetu alitega maeneo korofi ya machangudoa ya Kinondoni-Makaburini, Viwanja vya Leaders Club, Mwananyamala na Ufukwe wa Coco jijini hapa.
Maeneo ya Kinondoni-Makaburini, mwandishi huyo aliungana na machangu hao waliochanganyika na mashoga, ambapo aliwadanganya anatokea Buguruni na kwamba, kule biashara haikuwa nzuri.
Wakongwe wa biashara hiyo maeneo hayo walimtaka mwandishi huyo kuwa mpole hadi wenyewe wakishapata wateja ndipo naye ajiuze na siyo kujionesha kwa wateja kwani angewafunika kwa kuwa walidai ni mzuri kuliko wao.
HUYU HAPA MWENYEWE AKIWA KINONDONI
“Kiukweli siku hiyo walisema hakukuwa na wanaume na kwamba, hali kwa sasa ni ngumu. Pesa hakuna kutokana na Rais Magufuli (John Pombe) kubana matumizi serikalini.
“Walisema hali ni tofauti na serikali iliyopita kwa sababu wanaume walikuwa wa kumwaga, walikuwa wakikata mkwanja mzuri lakini sasa akitokea mwanaume mmoja hata kama akitaka kuondoka nao wote akalale nao kwa mpigo ndiyo pona yao ilimradi tu akate mshiko,” anasimulia mwandishi huyo na kuongeza:
“Wanasema wanachokipata siyo kwamba wanakwenda kutumia kwa anasa bali kujikimu mahitaji ya kifamilia.
Wengine wanalea watoto, wanasomesha, wengine wana wagonjwa wanaowategemea kuwalipia matibabu.
“Lakini yupo mmoja aliniambia amejenga nyumba Kigamboni kwa pesa hiyohiyo aliyopata kwa kujiuza.”
HITIMISHO LA JUMATATU
Hata hivyo, siku hiyo haikuwa nzuri kwani ilipofika usiku wa manane, machangu hao walikata tamaa na kurudi majumbani mwao wakilalamika kuwa, Magufuli anawaua njaa.
SIKU YA PILI, MANZESE
Siku iliyofuata, Jumanne, mwandishi wetu alifunga safari hadi Manzese Tip Top na baadaye Uwanja wa Fisi. Huko hali aliyoishuhudia ilikuwa ni zaidi ya kilichokuwa kikifanyika enzi za Firauni au Sodoma na Gomora.
“Kule nilishuhudia watoto wa umri wa miaka 12 hadi 15 wakiuzwa na kujiuza kwa ‘mijibaba’ sawa na baba au babu zao.
“Tofauti na Kinondoni ambako wanaojiuza wengi ni watu wazima, kule Manzese na Tip Top hali ilikuwa tofauti. Kuna watoto wadogo wanaouzwa na wamama watu wazima kwa wanaume na pesa wanachukua wanawake hao.
“Kumbe kwa Manzese kuna vibinti vidogo vinauzwa kwa ajili ya ngono! Kiukweli nilifuatwa na wanaume wengi lakini kwa kuwa nilikuwa kwenye kazi maalum niliwakatisha tamaa kwa kuwatajia dau kubwa.
“Wengine walinitukana, walidai ninaringa wakati sina lolote lakini wapo waliosema kwamba wachangishane ‘wakanishughulikie’ kwa zamu.
ATOROKA SOKONI
“Nilipoona mazingira hayo hayakuwa na usalama wa kutosha kwangu, nilitoroka kwa bodaboda kuinusuru roho yangu.
SIKU YA TATU, SINZA
“Siku ya tatu ya kazi yangu, Jumatano sasa, nilizamia mitaa ya Sinza nikianzia Afrika Sana, Sinza-Mori (barabara ya kuelekea Meeda Bar) na kufanikiwa ‘kujiuza’ nao licha ya kuwa walikuwa wakali mno na hawakutaka mgeni kwenye eneo lao.
“Nilijaribu kuwauliza maeneo hayo kuna usalama? Maana huko Kinondoni nilikokuwa kamatakamata ya Makonda ni noma. Wenyewe walisema tatizo njaa,” anazidi kusimulia mwandishi wetu.
“Nikiwa maeneo ya Sinza-Mori, nakumbuka ilikuwa usiku mnene. Awali nilipofika waliniambia; ‘wewe dada ni mzuri jamani, tumekupenda. Na wewe ni changudoa wa hapa?’ Niliwajibu hapana ni wa eneo jingine! Wakataka kunifukuza lakini mmoja wao aliniombea kwa wenzake kwamba nikae tu kwenye kiti kwani nikisimama nitawazibia biashara yao, yaani wateja wataniona mimi zaidi.”
APEWA KITI
“Kweli nilikubali kukaa pembeni kwenye kiti huku nikijifunza mazingira ya utendaji wao wa kazi. Kimsingi walionekana kutotulia sehemu moja badala yake walikuwa wakirandaranda kuingia na kutoka kwenye baa iliyopo jirani na gesti moja maeneo hayo.
OFM WATOKEA, WALAMBA PICHA
“Kwa vile kila sehemu ilikuwa lazima nipigwe picha za ushahidi wa kazi yangu na wenzangu wa OFM, kwa hiyo hata pale walitokea wakiwa ndani ya gari ambapo walipiga picha nikiwa na machangudoa wale. Hapo ndipo upepo ulipobadilika. Mmoja wa wanawake watano aliwaambia wenzake kuna uwezekano nikawa nafahamiana na watu waliopiga picha.
“Kiukweli walinizidi nguvu kwa sababu, kwanza wana miili mikubwa kuliko mimi. Pia walionekana kudata vibaya mno. Kunirukia na kuninyang’anya simu haikuwa kazi kubwa kwao. Hicho ndicho kilichofuata.
“Waliipekua simu yangu baada ya kunitishia wakishinikiza niwape password. Huko ndiko walikokutana na meseji za kikazi na majina ya wasanii. Mmoja wao alihisi labda mimi ni msanii lakini walipokagua vizuri meseji ndipo wakagundua mimi ni mwandishi na kwamba nilikuwa pale kwa ajili ya upelelezi.
“Walidai walishafika watu wengi wa aina yangu hivyo huwa wako makini na mtu mgeni. Ndipo wakaanza kuniburuza hadi ndani ya gesti hiyo kwa ajili ya kwenda kunifanyia kitu kibaya.”
NI TUKIO LA FEDHEHA
“Tulipofika ndani, mmoja wao alishauri wanipige picha nikiwa nusu utupu. Hilo likapita. Mmoja wao alinilazimisha kumbusu huku wakiniwekea kondom mabegani na mwingine alinipiga picha. Kwa vile nilikuwa chini ya ulinzi wao, sikutaka kupingana nao kwa mabavu.
“Baadaye waliniingiza kwenye moja ya vyumba vyao katika gesti hiyo. Nilichokikuta ni aibu na ukatili ulionifanya niamini kuwa, ulikuwa ndiyo mwisho wa maisha yangu.
“Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea, tayari nilishawapa taarifa OFM kwa njia ya siri kuwa nimenaswa, kwani hawakuwa mbali na eneo la tukio, nao wakatoa taarifa polisi ambao walifika na kunikomboa nikiwa salama kabisa,” hivyo ndivyo alivyohitimisha uchunguzi wake mwandishi wetu.