CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba Mkutano Mkuu Maalumu wa chama
hicho, utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii si wa kupokezana vijiti, kwa
sababu nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti unapofika wakati wa
uchaguzi haziombwi, bali yanapendekezwa majina ya watu wanaofaa kushika
nyadhifa huo.
Aidha, kimesema maandalizi ya mkutano huo utakaofanyika Jumamosi wiki hii, yamekamilika na unatarajiwa kushirikisha wajumbe 2,456 na mpaka sasa wamekodi hoteli 306 ambazo zitawalaza zaidi ya watu 3,331 mjini Dodoma.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari jana, Msemaji wa CCM, Christopher
ole Sendeka alisema Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa utamchagua Mwenyekiti
wa CCM Taifa baada ya Mwenyekiti wa sasa, Jakaya Kikwete kung’atuka na
kutoa nafasi hiyo kwa Rais John Magufuli kugombea.
Alisema
Rais Magufuli atakuwa Mwenyekiti wa CCM wa tano baada ya Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete.
“Kwa
mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya Mwenyekiti wa CCM na Makamu
Mwenyekiti wawili unapofikia wakati wa uchaguzi nafasi hizi haziombwi
isipokuwa Kamati Kuu inafikiria na kupendekeza majina na kuyawasilisha
kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo humteua,” alisema Sendeka.
Alisema
kisha Mkutano Mkuu wa Taifa unamchagua kwa kumpigia kura. Alisema
wanaopendekezwa hawajazi fomu za kugombea nafasi hizo na katika mchakato
huo kinachofanyika si kupokezana kijiti, kama wengi wanavyopenda kuita,
bali ni uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa CCM.
Alisema
katika uchaguzi huo itapigwa kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’ ili kupata
mwenyekiti na lazima apate nusu ya kura na akipata chini ya nusu
mapendekezo yataanza upya.
“Tuna imani wajumbe wote watampa mwenyekiti mpya kura zote za ‘ndio’ ili achukue nafasi ya kuongoza kitaifa,”
alisema na kuongeza kuwa akipatikana mwenyekiti ataunda ‘jeshi’ lake,
kwani hiyo ni desturi ya chama na walio katika Sektetarieti, watapisha
ili mwenyekiti mpya aunde jeshi lake.
Rais
Magufuli anatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya CCM
baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa Taifa, kwa kupanga upya safu yake ya
viongozi, ambao anaamini anaweza kufanya kazi nao kwa ajili ya kuleta
mabadiliko ndani ya Chama.
Viongozi
watakaojiuzulu ili kupisha Dk Magufuli kupanga safu hiyo ni Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana, manaibu katibu mkuu wawili na watendaji
wengine.
Wajumbe
wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni pamoja na Katibu Mkuu,
Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Katibu wa
Oganaizesheni, Katibu wa Siasa na Uhusiano ya Kimataifa, Katibu wa
Uchumi na Fedha na wa Itikadi na Uenezi.
“Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana atakabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa
chama kupisha Rais Magufuli aweze kuunda safu yake ya watu atakaofanya
nao kazi,” alieleza Sendeka na kuongeza kuwa anaamini Magufuli ataunda safu nzuri itakayoleta mabadiliko.
“Chama madhubuti huzaa serikali madhubuti na chama legelege huzaa serikali legelege,” aliongeza
na kubainisha kuwa maandalizi kwa ajili ya mkutano huo, yamekamilika na
tayari fedha zimetumwa mikoani ili kuwezesha wajumbe wote kufika; na
magari yatakodishwa kuwaleta mjini hapa.
Alisema
jumla ya wajumbe 2,456 watahudhuria mkutano huo, lakini pia
wanajitahidi kuweka hesabu vizuri kwa kuondoa wajumbe wenye kofia mbili.
Alisema wamekodi hoteli 306. Akizungumzia hali ya usalama alisema
wamejipanga kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa amani.
“Dodoma ni shwari na salama watu wasiwe na hofu na tuna imani mkutano utamalizika vizuri,”
alifafanua na kuongeza kuwa wajumbe wa NEC watawasili Alhamisi tayari
kwa kikao cha Ijumaa na wajumbe wengine watawasili Ijumaa.