Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi kisichojulikana
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la
Nay wa Mitego hadi hapo litakapojiridhisha kwamba ametekeleza maagizo
yote aliyopewa na Baraza sambamba na yeye kubadilika katika kubuni kazi
zenye maadili na zisizo dhalilisha watu wa kada mbalimbali.
Maagizo
aliyopewa Msanii Nay ni pamoja na kulipa faini (adhabu) ya kiasi cha
Shilingi milioni 1, kufanya marekebisho ya mashairi ya wimbo wake wa
‘Pale Kati’, kufuata sheria, kanuni na taratibu za urasmishaji sekta ya
Sanaa kwa maana ya kusajiliwa na BASATA na kuhakikisha wimbo wake
umefuata taratibu zote.
Aidha,
Msanii Nay ameagizwa kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi ya muziki
yenye kuvunja maadili na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali hususan
wanawake.
Maamuzi
haya yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria nambari 23
ya mwaka 1984, ikisomwa pamoja na kifungu cha 30(1)(2) na waraka wa
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wa tarehe 16/7/2009 ambayo kwa
sasa inafahamika kama Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Adhabu
hizi zimetolewa kufuatia BASATA kufanya kikao cha pamoja na Msanii huyu
jana siku ya Jumanne tarehe 26/07/2016 kwenye Ukumbi wa Baraza na yeye
kukiri makosa na kuahidi kubadilika.
Makosa aliyosomewa na yeye kuyakiri kwa maandishi ni pamoja na;
1. Kujihusisha na shughuli za Sanaa pasipo kusajiliwa na BASATA.
2. Kutoa wimbo wa “Pale Kati” na kuupakia katika mitandao ya kijamii bila kuuleta kufanyiwa uhakiki wa maudhui yake.
3.
Maudhui ya wimbo wa ‘Pale Kati’ kwa sehemu kubwa hayafai kwa matumizi
ya wazi na ni kinyume cha sheria za nchi na maadili ya mtanzania.
Ikumbukwe
kwamba mnamo tarehe 16/07/2016 BASATA lilitoa taarifa kwa umma ya
kuufungia wimbo wa Pale Kati kufuatia kubeba maudhui yenye uvunjifu
mkubwa wa maadili na kupambwa na picha dhalilishi kwa wanawake.
Aidha,
tarehe 12/02/2016 BASATA liliufungia wimbo wa Shika Adabu Yako wa
Msanii huyuhuyu kwa makosa yanayofanana na haya. Hivyo adhabu hii
imetolewa ili kumpa muda wa kujifunza, kujitathimi na kujirekebisha kama
kweli ana nia ya kuendelea kufanya kazi ya muziki
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA.