Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akikabidhi mbuzi wawili,mchele kilo 100 na mafuta ya kupikia lita 20 kwenye kambi ya kulea wazee wasiojiweza iliyopo Kolandoto katika manispaa ya Shinyanga kwa ajiri ya kusheherekea sikukuu ya Eid el Fitri kwa niaba ya rais John Pombe Magufuli ambaye ndiye aliyetuma zawadi hizo wapelekewe wazee hao.
Afisa mfawidhi wa kambi hiyo ya wazee wasiojiweza Sophia Kang'ombe akimpokea katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela na kupokea zawadi hizo kwa ajiri ya wazee hao kufurahia sikukuu hiyo ya Eid El Fitri kama watu wengine walioko majumbani.
Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akizungumza kwenye kambi hiyo ya wazee ambapo ameahidi serikali kuendelea kuwatatulia changamoto ambazo zinawakabili ikiwa baadhi yao zimefanyiwa kazi kama vile kuwepo kwa maji safi na salama, umeme kufungwa pamoja na kupatiwa matibabu kwa kiwango kizuri na kuwafanyia utaratibu wa kupata kadi za bima ya afya.
Mwenyekiti wa kambi ya Kolandoto Samweli Maganga akipokea zawadi ya chakula na kitoweo huku akimshukuru Rais Magufuli kwa kuthamini makundi maalumu, ambapo pia alimuombea aishi maisha marefu yenye baraka na afya tele akisema ni mtu aliyeletwa na mwenyezi mungu kuwakomboa watu wanyonge ambao walikuwa wamesahaurika kwa miaka mingi
Kambi ya wazee ya Kolandoto inalea wazee 23 pamoja na watoto wao na wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ubovu wa majengo ambayo baadhi yamesha anza kuanguka menyewe sababu ya kuchakaa na hivyo kuhofia usalama wa maisha yao.
Akizungumza baada ya kupokea zawadi hiyo ya chakula,mwenyekiti wa wazee hao mzee Samweli Maganga alisema anampongeza Rais Magufuli kwa kujali makundi maalumu huku akiiomba serikali kuwajengea majengo mapya kwani yaliyopo yameshachakaa.
“Tunaipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya rais Magufuli hasa kwa kujali makundi maalumu kwa kututatulia changamoto zetu, baadhi ya changamoto zimeshatatuliwa mfano hivi sasa tumefungiwa umeme, maji yapo na suala la matibabu hatupati shida kama zamani, tunaamini na kero hii ya majengo mabovu itatatuliwa tu”,alisema Maganga.
"Kutokana na utendaji kazi anaouonesha rais Magufuli, tunamuombea kwa mwenyezi mungu aendelee kuinyoosha nchi katika uimara wake na aiishi maisha marefu bila hata ya kupata maradhi wala vikwazo maana ni mkombozi wa watu wanyonge”,aliongeza Mzee Maganga.
Akikabidhi chakula hicho kwa niaba ya rais Magufuli katibu tawala la mkoa wa Shinyanga Albert Msovela alisema wametoa mchele kilo 100, mafuta lita 20 pamoja na mbuzi wawili na kuongeza kuwa serikali itaendelea kuzitatua changamoto za wazee moja baada ya nyingine ili kuhakikisha wazee wanaishi mahali salama.
Naye mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe ambaye aliambatana na katibu tawala huyo kukabidhi zawadi hizo za chakula kambini hapo, alisema pia serikali itafanya mkakati wa kuhakikisha wazee hao wanapatiwa kadi za bima ya afya ambazo zitawasaidia kupata matibabu kwa urahisi.
Na Marco Maduhu- Msukuma Blog