Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kuwaondoa watumishi wote
wasiokuwa askari polisi na ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya
ukiukwaji wa taratibu na ufujaji wa fedha za umma ili kulinda heshima,
nidhamu na uadilifu ndani ya jeshi hilo.
Rais Magufuli ametoa maelekezo hayo leo tarehe 18 Julai, 2016 muda
mfupi baada ya Naibu Makamishna wa Polisi 25 na Makamishna Wasaidizi
Waandamizi wa Polisi 35 kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma,
Ikulu Jijini Dar es salaam.
Pamoja na kutoa agizo la kutaka wasio askari polisi kuondolewa katika
utumishi wa jeshi la polisi, Rais Magufuli pia ameagiza jeshi hilo
lichukue hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha
wakiwemo wanaodaiwa kuiba mabilioni ya shilingi zilizotolewa kwa ajili
ya ununuzi wa sare za askari mwaka jana 2015.
"Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, ofisi ya IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) ipo palepale, ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) ipo palepale, Makamishna wote mnazunguka mnakwenda palepale, mwizi mnae palepale, mnashindwa kumshika.
"Kama mnafikiri kuwa na raia katika jeshi la polisi
wanawaharibia kazi zenu hamisheni raia wote na wapelekeni utumishi,
kwani hakuna mhasibu ambaye ni askari polisi? hakuna mhandisi ambaye ni
askari polisi? hakuna afisa tawala ambaye ni askari polisi? Mimi
nafikiri kama matatizo ya wizi na wafanyakazi hewa yanaletwa na raia
waliomo ndani ya jeshi la polisi na majeshi yetu mengine, IGP
kaorodheshe raia wote wanafanya kazi Jeshi la Polisi ili waondolewe na
tuwapangie kazi nyingine uraiani" Amesema Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri
linayofanya iliyoliwezesha kujenga imani kubwa kwa watanzania na ametaka
viongozi wa Jeshi hilo wawaongoze askari walio chini yao vizuri,
wawatie moyo na waache vitendo vya kuwakatisha tamaa kwa kuwaadhibu ama
kuwatisha pale wanapochukua hatua stahiki dhidi watu wanaovunja sheria.
"Sasa mimi niwaombe nyinyi, wale wadogo mnaowaongoza
mkawape mamlaka ya kutimiza wajibu wao, hata kama ameshika gari la IGP
liache lishikwe IGP atakwenda kujieleza mwenyewe, hata akishika gari la
RPC afanye hivyohivyo, hata akishika gari la Waziri au gari la Rais
mwacheni atekeleze wajibu wake, sheria ni msumeno, tunawanyima nguvu
hawa wa chini wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria halafu
unamwambia liachie, ukifanya hivyo aliyeshikwa anatoka pale akiwa
anatamba kwelikweli na yule askari unamvunja nguvu ya kufanya kazi" Amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amelitaka jeshi hilo kuungana na vyombo vingine vya
serikali katika kutekeleza shughuli zake zikiwemo kusimamia ukusanyaji
wa mapato ya serikali bandarini, katika sekta ya utalii na maeneo
mengine, kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuondoa watumishi hewa.
Tukio hili la Naibu Makamishna wa Polisi na Makamishna Wasaidizi
Waandamizi wa Polisi kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma
limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na
limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Utumishi na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mhe. George Mcheche Masaju, Makatibu Wakuu na Viongozi wa vyombo vya
Ulinzi na Usalama.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016
Social Plugin