Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
30 Julai, 2016 ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Tabora akitokea
Mkoa wa Singida.
Kabla
ya kuingia Mkoani Tabora, Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mji
wa Misigiri katika Wilaya ya Iramba ambapo amemuagiza Meneja wa Wakala
wa Barabara katika Mkoa wa Singida kuhakikisha mkandarasi anayejenga
daraja la Sibiti anarejea kazini mara moja kukamilisha ujenzi wa daraja
hilo.
Rais
Magufuli amesema serikali yake imejipanga kumlipa fedha mkandarasi huyo
na hivyo hakuna sababu ya kuendelea kusimamisha ujenzi huo.
Mkoani
Tabora, Rais Magufuli amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara
wake katika vijiji vya Nanga na Ziba na amefanya mikutano ya hadhara
katika miji ya Igunga na Nzega ambako amewahakikishia wananchi kuwa
serikali yake itahakikisha inatekeleza ahadi zilizopo katika Ilani ya
Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2015.
Katika
mkutano wa hadhara uliofanyika Igunga, Rais Magufuli amepokea
malalamiko ya wananchi kuhusu kutoanza kutumika kwa kituo cha mabasi na
soko na amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha kituo cha
mabasi cha Igunga na soko la Igunga vinaanza kutumika kuanzia Jumatatu
ijayo ya tarehe 01 Agosti, 2016.
Kuhusu
kero ya maji, Dkt. Magufuli amesema Tanzania imepata mkopo wa dola za
kimarekani Milioni 268.35 kutoka nchini India ambazo zitatumika
kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya ziwa Viktoria katika Miji ya
Tabora, Igunga, Nzega, Sikonge na Uyui pamoja na vijiji vilivyopo
kandokando mwa bomba kuu kuanzia mwaka huu ambapo watu milioni moja na
laki moja (1,100,000) watanufaika.
Dkt.
Magufuli ameongeza kuwa pamoja na juhudi hizo Serikali imefanya usanifu
na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya
kutoka mto Malagarasi kwa ajili ya Miji ya Urambo, Kaliua na Nguruka
pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu ambako watu laki
sita (600,000) watanufaika.
Aidha, Rais Magufuli amepiga marufuku wakulima wadogo kutozwa ushuru wa mazao watokapo na mazao mashambani.
“Ninapenda
tukusanye kodi, lakini sio kukusanya kodi kutoka kwa watu masikini, mtu
ametoka shambani na magunia yake mawili au hata matano halafu nyinyi
mnamtoza kodi.
“Mimi
sipendi kuwanyanyasa hawa watu wanyonge, mtu akiwa na mazao lori zima
hapo sawa lakini sio kwa mtu mnyonge mwenye gunia moja” Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu
maombi ya Mkoa wa Tabora kutaka kuanzishwa Mkoa mwingine kutokana na
ukubwa wa baadhi ya Wilaya Rais Magufuli amesema haoni umuhimu wa
kuanzisha Mikoa mipya hapa nchini kwa sasa, na badala yake fedha
zitaelekezwa katika huduma kwa wananchi kama vile maji, barabara,
miundombinu na huduma za afya.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Nzega
30 Julai, 2016