Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Serikali Yaifuta Bodi ya Ushirika Kagera..Viongozi Wake Wasimamishwa Kazi

Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Kagera, Kagera Co operative Union 1990 LTD (KCU) pamoja na Meneja Mkuu wa Chama hicho na Mrajisi Masidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera wamesimamishwa kazi kuanzia jana tarehe 21.07.2016 kwa tuhuma za ubadhilifu zaidi ya shilingi milioni 900 pamoja na kuingia mikataba yenye harufu ya rushwa iliyopelekea hasara kubwa kwa Chama hicho Kikuu cha Ushirika Mkoani Kagera.

Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Nchini Dkt. Audax Peter Rutabanzibwa akitangza rasmi kusimamishwa kwa Bodi ya KCU pamoja na Meneja Mkuu wa Chama hicho cha Ushirika alisema kuwa Bodi hiyo ikishirikiana na Meneja Mkuu Bw. Vedastus Ngaiza walitoa taarifa za uongo katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho wa mwezi Mei 2016 kuhusu deni wanalodaiwa na Benki ya CRDB.

Dkt. Rutabanzibwa alisema baada ya kutuma wakaguzi kutoka ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Wakaguzi hao walibaini kuwa taarifa waliyosomewa wananchama katika mkutano ilitaja kuwa deni lilikuwa Shilingi bilioni 2.8 kumbe haikuwa kweli kwani deni lilikuwa limepanda hadi shilingi bilioni 3.15 Bodi na Meneja Mkuu walikuwa wamewadanganya wanachama wa chama hicho.

Pili, Wakaguzi hao waligundua kuwa shilingi Milioni 124 zilitumika katika malipo na hakukuwa na maelezo ya kutosheleza kuhusu malipo ya fedha hizo. 
Tatu, KCU iliingia mikataba ya kukodisha majengo yake amabayo haikufuata bei ya soko kwa sasa, na mikataba hiyo ilifungwa kwa makubaliano ya miaka 10 jambo ambalo linapelekea Chama hicho kulipwa pango kwa bei ya chini kabisa isiyoendana na soko.

Nne, Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Kagera KCU kimekuwa kikinunua kahawa ya kiwango cha chini kabisa na kusababisha hasara kubwa. 
Tano, Chama cha KCU kilijiingiza katika miradi isiyokuwa na tija kama mradi wa kununua maharage ambao ulikisababishia hasara kubwa Chama hicho.

Dkt. Rutabanzibwa alisema kuwa kutokana na sheria Na. 6 ya mwaka 2003 inayohusu usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini Bodi ya KCU hakufanya  kazi yake ipasavyo ya kukisimamia vizuri chama hicho 
Aidha, Bodi hiyo ilifanya vikao 12 kwa mwaka jana 2015 vikao ambavyo vinaonekana havikuwa na tija kwani pamoja na vikao hivyo vya Bodi kufanyika bado kulikuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha.

MAELEKEZO
Dkt. Ruatabazibwa baada ya kutaja ubadhirifu uliofanyika katika Chama Kikuu cha Ushirika KCU alisema kuwa Serikali imeamua kuchuka hatua zifuatazo;

1. Kufuta Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Kagera KCU iliyoteuliwa mwaka 2014

2. Kusitisha ajira ya Meneja Mkuu wa KCU Bw. Vedastus Ngaiza mpaka hapo uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha utakapokamilika.

3. Kusitisha nafasi ya Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Kagera Bw. Nestory Shorozi kwani ubadhirifu huo ulifanika yeye akiwepo bila kukishauri vizuri Chama hicho Kikuu cha Ushirika .

4. Akaunti zote za Chama cha Ushirika KCU kusimamishwa mara moja mpaka hapo utaratiibu mzuri utakapokuwa umewekwa .

KUNUSURU CHAMA
Dkt. Rutabanzibwa alisema kuwa katika kukinusuru Chama Kikuu cha KCU pia na kuendelea na Msimu wa manunuzi ya kahawa Serikali imefanya uteuzi mdogo wa Mrajisi Msaidizi Bw, Robert Makene Mtambo kutoka Ukerewe Mkoani Mwanza atakayeshikiria kwa muda nafasi ya Bw. Nestory Shorozi aliyekuwa Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Kagera.

Aidha mrajisi Msaidizi aliyeteuliwa Bw. Mtambo atakaimu nafasi ya Meneja Mkuu wa KCU iliyokuwa ikishikiliwa na Bw. Vedastus Ngaiza. 
Katika kukaimu nafasi hiyo Bw. Mtambo atatakiwa kuitisha Mkutano Mkuu wa wanachama wa KCU ndani ya mwezi mmoja na katika mkutano huo atateuliwa Mwenyekiti ambaye atatakiwa kusoma taarifa halisi ya KCU iliyotakiwa kusomwa mwezi Mei 2016 katika Mkutano Mkuu.

Adha Dkt. Rutabanzibwa alisema Serikali haikukurupuka kuchukua hatua hiyo bali ilifanya uchunguzi wa kutosha ikiwa ni pamoja kuipa bodi nafasi ya kujieleza lakini haikutoa maelezo ya kutosha na badala ya kupunguza deni wao waliliongeza deni likapanda zaidi. 
Pia Dkt. Rutabanzibwa aliviagiza vyombo vya uchunguzi kama TAKUKURU, Polisi na Usalama kuanza kulifanyia kazi suala hilo mara moja.

Kaimu Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika Dkt. Audax Peter Rutabanzibwa alimalizia kwa kusema kuwa Serikali imeamua kulifanyia kazi suala la VyamaVikuu vya Ushirika nchini kwani vyama hivyo vimeonekana kuwa badala ya kuwasaidia wakulima vinawadidimiza ambapo alisema walianzia Mwanza, sasa Kagera, na wanaelekea Mikoa ya Geita, Simiyu, na Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com