TUME
ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza utaratibu mpya kwa watahiniwa
wa mwaka mpya wa masomo wa 2016/2017 wanaochukua shahada, huku wanafunzi
wengi wakiwa hatarini kukosa nafasi kwa kukosa sifa na vigezo.
Utaratibu
huo mpya umekuja ikiwa ni miezi miwili sasa tangu kutumbuliwa kwa
watendaji wa tume hiyo kutokana na kudahili wanafunzi wasio na sifa na
kusababisha kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB).
Sifa
hizo ziliwekwa mapema wiki hii katika tovuti ya TCU na kurudiwa jana.
Taarifa hiyo inaonyesha kutolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo,
Eliuta Mwageni.
Akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu jana, Ofisa Habari Mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku, alithibitisha taarifa ya utaratibu huo mpya.
Mkaku
alisema utaratibu huo umetolewa baada ya mwaka jana kutumika mfumo wa
wastani wa pointi (GPA) ambao Januari, mwaka huu, Waziri wa Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,
aliagiza ufutwe na kurudishwa ule wa madaraja (division) uliotumika siku
zote.
“Mfumo
wa udahili uliotumika mwaka jana ulikuwa ni GPA na mwaka huu utatumika
mfumo wa divisheni, ndiyo maana utaratibu huo ukawekwa,” alisema Mkaku.
Moja
ya sifa zinazotakiwa katika udahili wa mwaka huu wa masomo (2016/2017),
ni wahitimu wa kidato cha sita waliomaliza kabla ya mwaka 2014 kuwa na
ufaulu wa (D mbili) pointi 4.0.
Mchanganuo ulionyesha kuwa pointi hizo zinatokana na ufaulu wa A = 5; B= 4; C= 3; D = 2; E = 1.
Taarifa
hiyo ilionyesha kuwa ili wahitimu wa kidato cha sita kwa mwaka 2014 na
2015 wawe na sifa za kudahiliwa, watatakiwa kuwa na alama za ufaulu wa
(C mbili ) pointi 4.0 kupitia mchanganuo wa A = 5; B+ = 4; B = 3; C= 2; D
= 1.
Pia
tovuti hiyo ilionyesha kuwa wahitimu waliomaliza kidato cha sita kwa
mwaka huu, watahitajika kuwa na ufaulu wa alama (D mbili) 4.0 kupitia
mchanganuo wa A = 5; B = 4; C= 3; D= 2; E = 1.
Mbali
na sifa hizo, watakaodahiliwa ni wale ambao pia watakuwa na
utambulisho wa sifa za kielimu za kidato cha nne ambazo ni kuanzia alama
nne za D na kupanda juu katika mchanganuo wa alama za ufaulu wa B+,
ikiwa A =75-100, B+ = 65-74, B=50-64, C=40-49, D=35-39, F= 0-38.
Sifa
nyingine zinazotakiwa ni wenye cheti cha NVA daraja la tatu pamoja na
ufaulu wa si chini ya alama nne za D za kidato cha nne au sifa nyingine
zinazokaribiana na hizo, ikiwa ni pamoja na zinazotambuliwa na Baraza la
Taifa la Mitihani (NECTA) au Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi (VETA).
Pia
watahiniwa hao watatakiwa kuwa na angalau GPA ya 3.5 kwa stashahada
(NTA) daraja la sita au wastani wa B kwa cheti cha ufundi (FTC) katika
mchanganuo wa alama A=5, B=4, C=3 na D=2 au wastani wa daraja la B+ kwa
wenye stashahada za ualimu, au wastani wa daraja la B+ kwa kitengo cha
afya kama tabibu wa magonjwa ya binadamu na nyingine au cheti na
stashahada nyinginezo.
Sifa nyingine zinazoangaliwa katika udahili huo ni kuwa na ufaulu wa daraja la pili kwa wenye stashahada zisizokuwa za NTA.
Pamoja
na hayo, TCU ilisema hakutakuwa na usajili wa mafunzo ya awali pamoja
na yale ya UQF6 yaliyozuiwa kuanzia mwaka wa masomo wa 2016/2017.
Taarifa
ya tovuti hiyo iliendelea kusema kuwa maombi yote ya usajili wa
wanafunzi hao wanaotaka kuchukua shahada yanatakiwa kupitia TCU pekee.
“Kwamba
tume hiyo imeamua kuwa kuanzia mwaka 2016/2017, maombi yote ya usajili
kwa makundi yote yanayoanzia aya ya 3.0 kwenda juu wataunganishwa na TCU
pekee na walio chini ya hapo hawatahusika na tume hiyo,” ilisema taarifa hiyo.
Pia
TCU ilisema taarifa hiyo ni kwa mujibu wa kipengele cha 5(1)(c)(i) cha
katiba ya vyuo vikuu, kifungu cha 346 cha sheria nchini.
“Msingi
wa kubadili viwango vya kujiunga na elimu ya juu ni kutokana na kuwepo
maoni kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya uwezo wa wahitimu wanaojiunga
na vyuo vikuu mbalimbali,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mei,
mwaka huu, Profesa Ndalichako aliwasimamisha kazi Katibu Mtendaji wa
TCU, Profesa Yunus Mgaya, kwa kushindwa kuisimamia tume hiyo kutokana na
kuwapo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa, kisha wakadahiliwa katika vyuo
vikuu na kupata mkopo.
Wengine
aliowasimamisha kazi ni Mkurugenzi wa Ithibati na Udhibiti Ubora, Dk.
Savinus Maronga, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kiishweko na Ofisa Msimamizi Mkuu wa Taarifa, Kimboka Stambuli.
Pia
Mei mwaka huu, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idrisa
Kikula, alitangaza kuwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi
maalumu ya stashahada ya ualimu ambao hawakuwa na sifa.
Alipozungumzia
sakata hilo Juni, mwaka huu wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa
ujenzi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Dk. John
Magufuli, aliwaita wanafunzi hao kuwa ni vilaza, na kwamba idadi kubwa
ya waliofukuzwa hawakuwa na sifa stahiki za kudahiliwa kusoma kozi
hiyo.
Social Plugin