Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye Akubali Kuwania Uenyekiti CHADEMA


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amekubali ombi la viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani, waliomchukulia fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho kanda hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.


Baadhi ya viongozi hao waliojitokeza kumchukulia fomu Sumaye ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, Mwenyekiti wa chama hicho Ilala, Dk. Makongoro Mahanga na Mwenyekiti wa mkoa wa Pwani, Baraka Mwago.


Baada ya kuchukua fomu hiyo katika ofisi za Chadema Kanda Kinondoni jana, viongozi hao walielekea nyumbani kwa Sumaye maeneo ya Tondoroni Kiluvya, mkoa wa Pwani, kwa ajili ya kumkabidhi.


Baada ya kupokea fomu hizo, Sumaye alikubali ombi hilo na kuzijaza na kuahidi kurejesha leo katika ofisi hizo.


Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake mara baada ya kukabidhiwa fomu hizo na Waitara, Sumaye alisema ni wakati sasa wa kukipeleka chama hicho hadi vitongojini.


Waziri Mkuu huyo mstaafu alihamia upinzania mwaka jana katika harakati za uchaguzi mkuu akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post