WAZIRI Mkuu wa India, Narendra Modi anawasili leo nchini kwa ajili ya ziara ya kitaifa ya siku mbili kwa lengo la kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema Modi atatumia fursa hiyo kukuza uhusiano wa kihistoria baina ya nchi hizi mbili pamoja na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi.
Alisema Modi atakutana na Rais John Magufuli Ikulu na kufanya naye mazungumzo. Pia kuweka saini kwenye mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya sekta za viwanda, maji, elimu, sayansi na teknolojia na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.
Dk Mahiga alisema Modi pia atazungumza na jumuiya ya wafanyabiashara wakubwa wa India ambao baadhi yao wameshaonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya ujenzi wa viwanda vya kutengeneza chuma, saruji, dawa ya binadamu na maji ya matunda.
“Natoa mwito kwa wafanyabiashara mbalimbali hapa nchini watumie fursa hii kushiriki ili waweze kukutana na wenzao, Kongamano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi,” alisema.