MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wilayani Urambo mkoani Tabora, imemuhukumu Deus Barnaba(45) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumkuta na hatia ya kumnajisi mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka tisa.
Akitoa hukumu hiyo mwishoni wa wiki iliyopita, Hakimu Mkazi, Baptista Kashusha, alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka hivyo kumuona mshitakiwa ana hatia.
Alisema adhabu hiyo iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kufanya vitendo hivyo. Hakimu Kashusha alisema mashahidi nane walioletwa mahakamani hapo walithibitisha kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo.
Mashahidi hao ni pamoja na daktari aliyempokea mlalamikaji na kutoa fomu namba tatu (PF3) iliyoonesha kuwa binti huyo aliumizwa katika sehemu za siri.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, ,Joseph Mbwana, alieleza mahakama hiyo kuwa Machi 27, mwaka huu, majira ya saa 2:00 usiku katika kijiji cha Mwangaza wilayani Urambo, Deus alimnajisi binti mwenye umri wa miaka tisa na kumsababishia maumivu makali katika sehemu zake za siri.
Aidha, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili kukomesha matendo ya ubakaji kabisa kwani mtuhumuwa anaonekana ni mtu mwenye akili timamu, alifanya hivyo kwa makusudi tu.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwakuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana wazazi, mke na watoto wanaomtegemea.
Social Plugin