Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Ahukumiwa Kifungo Jela Miaka 30 Kwa wizi wa Pikipiki Kwa Kutumia Kisu

Mahakama ya wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12 mkazi wa Iyunga jijini Mbeya Salumu Ngasa maarufu kama Uncle Mkomavu (32) kwa unyang’anyi wa kutumia silaha.
 
 
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mhakama ya wilaya ya Mbarali Alice Mkasela, mwendesha mashitaka wa Polisi Omary Nilahe aliiambia mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 26 mwaka huu majira ya saa tano asubuhi katika kijiji cha Machimbo kata ya Mapogoro wilayani Mbarali.

Nilahe alisema wakiwa kijijini Machimbo kijana Salum akitumia kisu aina ya Sime alimvamia na kisha kumpora pikipiki mkazi wa kijiji hicho Maulid Juma na kisha kukimbia nayo.

Alisema siku chache baada ya tukio hilo la unyang’anyi jeshi la polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa wilayani Mbozi mkoani Songwe na ndipo Aprili 8 mwaka huu akafikishwa katika mahakama ya wilaya Mbarali na kusomewa shitaka lililokuwa linamkabili.

Kutokana na vitendo vya unyang’anyi wa kutumia silaha kukithiri mkoani hapa hasa kwa upande wa pikipiki, mwendesha mashitaka Nilahe aliiomba mahakama kumpa adhabu kali mshitakiwa ili kutoa fundisho kwa wengine walio na tama ya kujipatia mali kwa njia ya mkato.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkasela alisema kutokana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, mshitakiwa atapaswa kfungwa jela miaka 30 na pia kuchapwa viboko 12.

Awali mshitakiwa Uncle Mkomavu aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu,akisema pamoja na kutegemewa na familia na ndugu wa karibu pia ni kosa lake la kwanza kutenda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com