Askari wa Upelelezi Auawa Kwa Kuchomwa Kisu Baa Jijini Mwanza



Kwamba tarehe 21.08.2016 majira ya 10:00 usiku katika eneo la Club ya Villa Park Resort kata ya Kirumba wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza, askari namba g.5092 pc John Nyange wa ofisi ya mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai mkoa wa Mwanza (RCO), aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali eneo la shingoni na mtu aliyekuwa ana ugomvi nae.


Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa na ugomvi wa muda mrefu na mtu aliyejulikana kwa jina Magina Hussein miaka [27] fundi computer msukuma na mkazi wa mtaa wa kigoto, ambapo marehemu alikuwa akimdai bwana Magina Hussein computer aina ya laptop. Ndipo usiku wa leo majira tajwa hapo juu walikutana eneo la Club ya Villa Park huku mtuhumiwa wa mauaji hayo ikisemekana kuwa alikuwa na wenzake watano ndipo walimvamia na kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni na kufariki dunia njiani wakati akipelekwa hospitali.


Marehemu kwa sasa alikuwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Stefano Moshi Memorial University College Cha Mjini Moshi, alikuwa anasomea shahada ya Sayansi ya Habari na Mawasiliano mwaka wa pili, aidha alirejea Mwanza baada ya kupata likizo kuja kuiangalia familia yake ndipo umauti ukamkuta.


Watuhumiwa sita akiwepo Magina Selemani ambaye alikuwa na ugomvi na marehemu pamoja na wenzake watano wamekamatwa, wapo katika mahojiano na jeshi la polisi huku uchunguzi kuhusiana na kifo hicho ukiwa bado unaendelea, pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani, mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya rufaa ya Bugando kwa uchunguzi.


Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza naibu kamishina wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wananchi wa jiji na mkoa wa Mwanza, kwamba jeshi la polisi mkoa wa Mwanza limesikitishwa na kifo cha askari huyu kwani limempoteza askari kijana ambaye bado jeshi lilikuwa linamtegemea.


Lakini pia anawataka watu wenye tabia za kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga wengine hadi kufikia kupoteza maisha kuwa wanafanya kosa la jinai, na kama watu wanadaiana wafuate taratibu za kisheria zilizowekwa ili kuepusha vifo vinavyoweza kuepukika, hivyo jeshi la polisi linawataka kuacha tabia hiyo mara moja kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


Imetolewa na:
Dcp: Ahmed Msangi
Kamanda wa polisi (m) Mwanza
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post