Askofu Sangu wa Jimbo la Shinyanga Aibukia "GAMBOSHI",Kijue Chanzo Cha Kuitwa "Makao Makuu ya Wachawi Tanzania"

Askofu Sangu akiwa na wanafunzi shule ya msingi Gamboshi


Wananchi wa kijiji cha Gamboshi wakitoa zawadi ya Mbuzi kwa Askofu wa kanisa Katoliki jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, alipofika kijijini hapo kwa ajili ya kuzindua kanisa Katoliki kigango cha Gamboshi. 


Askofu  Sangu akiwa na diwani Gamboshi Bahame Kaliwa. 
 
Askofu Sangu akila chakula na wananchi wa Gamboshi.

 *****
Gamboshi ni kijiji kinachopatika Kata ya Gamboshi wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu  ni  takribani kilometa 37 kutoka Makao makuu ya Mkoa wa Simiyu, Mjini Bariadi.



Gamboshi kinatambulika kama kijiji ambacho ndiko makao makuu ya wachawi Tanzania “ Ikulu ya wachawi Tanzania” kinaelezwa kuwa ni kijiji chenye maajabu makubwa. 

  Historia ya kijiji hiki iliyosambaa nchi nzima, ndiyo inaweza kufanya kuwa Gamboshi lisiwe jina geni kwako, kwa bahati mbaya au nzuri historia hiyo imekuwa siyo nzuri hata kidogo.


Kijiji hicho kinatambulika kwa kila mtanzania kuzidi hata jina la wilaya au mkoa.Waandishi wa habari mbalimbali hapa nchini baadhi yao wamefanikiwa kufika katika kijiji hicho na wengine kukwamia njiani.

Waliofanikiwa kufika ndiyo wamesababisha Gamboshi kujulikana kwa kiwango hicho, lakini pia baadhi ya wananchi ambao baadhi yao ni wazawa wamekuwa wakitoa simulizi za kijiji hicho kupitia vyombo vya habari.

Simulizi na habari hizo zinaeleza kuwa kijiji hicho kimejaa mauza uza (miujiza), ukifika usiku Gamboshi inabadilika inaonekana kama mmoja wa mji mkubwa (Cairo), nyumba nyingi zenye ghorofa zaidi ya 50.


“Mchana kijiji hicho kinaonekana kawaida, mandhari yake kawaida kabisa ya kijijini, nyumba za nyasi na fupi, lakini usiku kunabadilika kijiji kinaonekana kama jiji, taa za wakawaka, jiji linalonga’aa” inasema moja ya simulizi.


Kutokana na historia ya Gambosi kuwa ya kutisha na ambayo imesambaa nchi nzima, inaelezwa kuwa toka Tanzania ipate uhuru hakuna kiongozi yeyote wa dini au serikali mkuu ambaye amefika.


Julai 27, 2016 ni siku ambayo wananchi wa kijiji hicho wanapata furaha ambayo inayotajwa kuwa haijawahi kuonekana, ni siku ambayo Askofu wa kanisa Katoliki jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu anakanyaga ardhi ya Gamboshi.


Askofu Sangu anafika kijiji hapo kwa ajili ya kuzindua Kanisa Katoliki Kigango cha Gamboshi, inaelezwa kuwa kanisa hilo limejengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji hicho, hali inayoshangaza kidogo.


Furaha kubwa ya wananchi wa GambosHi mara baada ya kuwasili kwa kiongozi huyo inaashiria jambo, wanasema haijawahi kutokea Kiongozi mkubwa wa serikali hata dini kufika kijijini hapo.


“Historia mbaya ambayo imekuwa ikituandama imetufanya kuonekana watu ambao siyo watanzania, tunaishi kisiwani, toka tumepata uhuru huyu ndiye kiongozi wa juu wa kwanza kukanyaga hapa Gambosi”, anasema Magreth Magesa
Umati mkubwa wa wananchi wa kijiji hicho pamoja na wanafunzi unafurika kanisani hapo kwa ajili ya kumuona Askofu Sangu, huku wengine wakitamani kumshika hata mkono au nguo zake.


Wakati mwingine Askofu Sangu alijikuta amezungukwa na umati mkubwa wa watu, huku wasaidizi wake wakishindwa kuwazuia kutokana na furaha waliyonayo akiwemo na askofu mwenyewe.


“Haijawahi kutokea hata siku moja, historia imetufanya kuwa watu wanyonge kila sehemu, unapotoka nje ya Gamboshi ukaelekea sehemu nyingine wakati mwingine unalazimika usitaje unapotoka”, anaeleza Paschal Charles.


Wananchi hao wanaeleza kuwa ujio wa kiongonzi huyo ni neema kubwa kwao na unakuwa mwanzo wa kuweza kubadilisha mawazo hasi ya watanzania juu ya kijiji chao ambayo yamedumu vichwani mwao.
Wanabainisha kuwa siyo kweli Gamboshi kuwa ni makao makuu ya wachawi, badala yake wanaeleza hapo zamani zilikuwepo familia mbili ambazo zilikuwa zikishindana kwa uchawi.

Wanaeleza familia hizo ni Mwanamabula na Mwanamakulyu, ambao walikuwa wakishindana kwa uchawi hali ambayo ilikuwa ikiwavutia watu mbalimbali hapa nchini kufika kijijini hapo kwa ajili ya kuchukua dawa.


“ Waliokuwa wakichukua dawa ndiyo waliopeleka habari hizi mbaya kwa watanzania wengine, toka zamani hiyo mpaka leo historia haijafutika, bado watanzania wameendelea kuamini Gamboshi ni ikulu ya wachawi” ,anasema Charles.
Bahame Kaliwa ni diwani kata ya Gamboshi aliyeshiriki hafla ya uzinduzi wa kanisa hilo, anasema licha ya umbali kuwa kilometa 37 kutoka mjini Bariadi makao makuu ya mkoa hakuna kiongozi yeyote wa mkoa ambaye amefika Gamboshi.


Bahame alieleza kuwa toka mwaka 2012 mkoa wa Simyu kuanzishwa hakuna mkuu wa mkoa ambaye amefika kijijini hapo, kutokana na historia mbaya inayotangazwa juu ya kijiji chake ndicho chanzo cha viongozi kutofika.


“ Leo ni shangwe kubwa kwetu wanakijiji, ni jambo la kihistoria Baba askofu kufika Gamboshi, hii itafuta historia mbaya inayotuandama toka zamani mpaka leo, ukweli Gamboshi ni sehemu sahihi, tulivu na wananchi wake siyo wachawi bali ni wacha mungu”, anaeleza Kaliwa

Kaliwa anaupongeza uongozi wa dini hiyo kuanzisha kanisa hilo, ambalo alieleza litafuta historia mbaya kwa wananchi wa Gamboshi kwa kutambulisha kuwa ni watu wanaomtegemea mungu na siyo uchawi.


“ Tumekuwa tukiumia na kukerwa kuitwa ikulu ya wachawi, tunataka kuwaambia watanzania kuwa sasa GambosHi na sehemu salama na watu wake wanamtegemea mungu na siyo uchawi kama inavyoelezwa” ,anaeleza Magreth Magesa mkazi wa Gamboshi.


John Mkinga ni Padri parokia ya Ngulyati ambapo Gamboshi ni eneo lake la kazi, anasema ambacho kimekuwa kikiongelewa juu ya kijiji hicho siyo kweli, huku akibainisha kuwa maisha kwa sasa yamebadilika kijijini hapo.

Padri John anabainisha wakati anaanza kazi katika parokia hiyo alipata wakati mgumu kuanzisha kanisa kijijini hapo, baada ya wananchi kumtaka aondoke huku akiulizwa kwa nini yeye ni mnene?.


“ Haikuwa kazi rahisi kufika mpaka hapa, hapa hapakuwepo kanisa bali tulikuwa tunasali chini ya mti (huo hapo), nilianza na waumini 10 tu, nilipofika hapa swali la kwanza niliulizwa na wanakijiji kwa nini nimenenepa?” ,anaeleza


Alibainisha kuwa alitumia mbinu mbalimbali zikiwemo kujumuika nao katika shuguli za maendeleo na burudani, lengo likiwa kutaka kubadilisha mienendo yao na kuanza kumtegemea mungu.

Hata hivyo anasema kuwa aliwashawishi hadi kufanikiwa na kuanza harakati za ujenzi wa kanisa, ambalo alieleza ndilo linazinduliwa na Askofu Sangu, huku likiwa na wahumini zaidi ya 200 kutoka 10.

Katekista Thomas Masenema ndiye kiongozi wa dini wa kanisa hilo, anaeleza kuwa amekuwa akishangaa maelezo yaliyoko mitaani kuwa tofauti sana na maisha ya kijijini hapo.


Anaeleza toka amefika Gamboshi kwa ajili ya kufanya kazi hiyo hajawahi kuona yale ambayo yanaelezwa ikiwemo kijiji hicho kubadilika inapofika nyakati za usiku pamoja na kuwa na wachawi wengi.


“ Niko hapa zaidi ya miaka 3, nafanya kazi vizuri naishi hapa, sijawahi kuona hayo ambayo yanasemwa, Gamboshi ni kijiji kama vijiji vingine, ni kweli uchawi ulikuwa lakini ilikuwa zamani” ,anasema Masenema.


Kutajwa kuwa ni kiongozi wa juu wa dini na wa kwanza kufika Gambosi kunaonekana kumshangaza Askofu Liberatus Sangu, ambapo anaeleza ni historia kubwa kwake na wananchi wa kijiji hicho.
Askofu Sangu anaeleza “ natamani kama ratiba ingelisema nilale hapa, mimi ningelilala, wala siogopi maneno ya watu, furaha yenu niliyoikuta na kuiona toka nimefika inanifanya nijiulizwe maswali mengi”

Anasema kuwa hali hiyo inamfanya kutoamini kuwa Gamboshi ni ikulu ya wachawi bali ni sehemu ambayo wananchi wake wanampenda mungu na kumtegemea kuliko inavyosemwa.


“ Mimi nimefurahi kukuta kumbe wananchi wa huku wanampenda mungu sana, nilipofika hapa sikuamini kama ni kweli na ambacho kimekuwa kikiandikwa katika vyombo vya habari, Ni kweli GambosHi siyo ikulu ya wachawi”, anasema .


Kiongozi huyo anawataka waandishi wa habari, viongozi wa dini, siasa na serikali kutumia nafasi zao katika kuhakikisha Gamboshi inasafishwa kwa kuwaeleza watanzani kuwa siyo ikulu ya wachawi tena.


Askofu Sangu anawataka wananchi wa Gamboshi kubadilisha tabia na maisha yao kwa kuanza kumtegemea mungu, huku akisisitiza kuwapeleka shule na kanisani watoto wao.
 

“ Ujumbe wangu mkubwa kwenu badilikeni sasa, kuweni watu wa mungu, wapelekeni watoto weni shule, pamoja na kanisani ili wakapate mafundisho yaliyo mema ya kujenga kijiji chenu”, anaeleza


Kiongozi huyo anahitimisha kwa kuwataka watanzania kuacha fikra hasi kwa kijiji hicho, huku akiwataka kuamini kuwa kijiji hicho siyo tena ikulu ya wachawi bali ni kijiji kinachomtegemea mungu.
 

Makala imeandaliwa na Derick Milton wa SIMIYU NEWS BLOG
 Soma zaidi >>><<HAPA>>

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post