Baraza
la Vyama vya Siasa nchini limesogeza tarehe ya mkutano wa kutafuta
suluhu ya operesheni Ukuta iliyotarajiwa kufanyika Septemba 1,2016
,kutoka Agosti 30 hadi Septemba 3 mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kaimu Mwenyekiti wa
baraza hilo Vuai Ally Vuai alisema mkutano huo umesogezwa hadi tarehe 3
na 4 Septemba,2016.
“Kamati ya uongozi leo tumekutana tena ili kufanya maandalizi ya mkutano tuliopanga kuufanya tarehe 30 na 31 mwezi huu.
“Tumepitia
list (orodha) ya wahudhuriaji, tumegundua siku zilizobaki kufikia
mkutano zisingetosha . Tumeamua kuusogeza mbali hadi tarehe 3 na 4,
Septemba mwaka huu ili mkutano uwe wa ufanisi,” alisema Vuai.
Aidha,
baadhi ya agenda zilizotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo ni
masuala ya amani na utulivu nchini pamoja na hali ya siasa kwa sasa.
Waandishi
wa habari walipohoji kwa nini baraza hilo lisifanye mkutano huo katika
tarehe zilizopangwa awali ili kutoa nafasi kwa wajumbe kujadili suala la
operesheni Ukuta ambayo imezua mabishano makali ya kisheria na kikatiba
kati ya serikali na Chadema, Cons Akitandi, Mwenyekiti wa fedha wa
baraza hilo alisema “kwanza ifahamike hatukutani kwa ajili ya Septemba
Mosi.”
“Upo
utaratibu wa kikanuni kwamba baraza lina vikao vya kila baada ya miezi
mitatu na vikao vya dharula. Haki haitapatikana katika mazingira ya
shari, wajumbe wanapaswa kutumia njia ya majadiliano na maridhiano
katika kufikia mwafaka,” alisema Akitandi.