Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungulia Msanii wa muziki wa kizazi
kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego kuendelea na
shughuli za Sanaa baada ya kuwa ametekeleza adhabu (maagizo) zote
alizopewa kama masharti ya kumfungulia.
Aidha,
BASATA kama mlezi wa wasanii linamfungulia kufuatia yeye mwenyewe (Nay
wa Mitego) kujutia na kukiri kwamba amejifunza na yuko tayari kubadilika
na kwamba hatarudia makosa aliyoyafanya.
Hata
hivyo, pamoja na kumfungulia kuendelea na shughuli za Sanaa Baraza
linamweka kwenye uangalizi maalum msanii huyo kama sehemu ya kuhakikisha
anaendesha shughuli za Sanaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
sambamba na kuzingatia maadili katika kazi zake.
Itakumbukwa
kwamba mnamo tarehe 27/07/2016 Baraza lilimfungia Msanii Nay wa Mitego
kwa kipindi kisichojulikana na kumtaka kutekeleza maagizo yafuatayo:
1.Kuhakikisha amesajiliwa na kuwa na kibali cha kuendesha shughuli za Sanaa
2. Kulipa faini ya shilingi milioni moja (1,000,000/-)
3. Kuomba radhi watanzania kupitia mkutano na waandishi wa habari na kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii
4. Kuufanyia marekebisho wimbo wa ‘Pale Kati’ ili ubebe maudhui yenye maadili
Msanii
Nay wa Mitego ametekeleza adhabu zote tajwa hapo juu. Leo hii
tunamkabidhi rasmi cheti chake cha usajili na kibali cha BASATA.
Hata
hivyo, pamoja na kuleta marekebisho mara mbili ya wimbo wa ‘Pale Kati’
Baraza bado halijaridhishwa na marekebisho hayo hivyo linaendelea
kuufungia wimbo huu hadi hapo litakapojiridhisha umekidhi vigezo vya
kimaadili.
Katika
kikao na Msanii Nay wa Mitego cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa
adhabu yake kilichofanyika tarehe 12/08/2016 Ofisi za BASATA ameagizwa
kuendelea kuufanyia marekebisho wimbo wake huo kama bado anaona
anauhitaji.
Baraza
linatoa maelekezo kwa vyombo vya habari na watanzania kwa ujumla kuacha
kuucheza wimbo huo hadi hapo itakapoelekezwa vinginevyo. Hatua na
adhabu za kisheria zitachukuliwa kwa chombo chochote cha habari
kitakachokiuka agizo hili.
Aidha,
katika kikao hicho cha tathimini ilibainika kwamba Msanii Nay wa Mitego
kwa taarifa potofu alizopewa alipanda Jukwaani kwenye tamasha la Mwendo
Kasi la tarehe 30/07/2016 akiwa katika adhabu. Kwa kosa hili ameandika
barua ya kuomba radhi na Baraza linafikiria hatua za kuchukua kwa
waandaaji wa tamasha hili.
Baraza
linatoa wito kwa wasanii kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu za uendeshaji shughuli za Sanaa sambamba na kuhakikisha
wanazingatia maadili katika kila kazi wanazobuni ili kuepuka matatizo
yasiyo ya lazima ambayo yanaathiri kazi zao kwa kiasi kikubwa sana.