Bilionea wa CHADEMA Atangaza Kutoa Trilioni 10 Kumuunga Mkono Rais Magufuli Serikali Kuhamia Dodoma

MFANYABIASHARA maarufu, Mustapha Jaffer Sabodo ametangaza kutoa dola za Marekani bilioni 5 (Sh trilioni 10) kwa ajili ya kuwekeza mkoani Dodoma, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono Rais John Magufuli kuhamisha makao makuu ya serikali kwenda mkoani humo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Sabodo alisema atawekeza kiasi hicho cha fedha, iwapo serikali yote itahamia mkoani humo, itakuwa ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alitamani kuona mkoa huo unakuwa makao makuu ya nchi.

Alisema alichofanya Rais Magufuli, kimewashinda marais wengine waliomtangulia, hivyo yeye kama mfanyabiashara na mtu mwenye mapenzi makubwa kwa nchi yake, lazima aunge mkono hatua hiyo ya Serikali kuhamia Dodoma ambayo aliita ‘Azimio la Dodoma’.

“Niliposikia anatangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba Serikali itahamia Dodoma, ilikuwa mara yangu ya kwanza baada ya miaka mingi kupita, nilitabasamu moyoni, jambo ambalo lilinitokea miaka 10 ya kwanza ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere. 

“Leo nimesikia kutoka kwako nimeona ile roho ya Nyerere imezaliwa tena. 

“Kwa hiyo natangaza kuunga mkono Azimo la Dodoma kwa kuwekeza dola za Marekani bilioni 5, ambazo zitatumika kwa ajili ya uwekezaji mkubwa katika huduma mbalimbali za jamii mkoani humo,” alisema Sabodo.

Sabodo alisema atatoa fedha hizo ili zitumike kuwekeza kwenye viwanda kama vya mvinyo, viwanda vya kusindika mihogo na viwanda vingine ambavyo vitahitajika katika mkoa huo.

Alisema kuwepo kwa huduma hizo mkoani Dodoma, kutasaidia kuufanya mji huo kukidhi matakwa ya watumishi wa umma watakaohamia huko.

Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa atafanya uwekezaji mkubwa huo kwa sababu lengo lake ni kuona mji wa Dodoma, unaungana na miji ya jirani kama Mpwapwa, Kondoa na Manyoni ili kutoa fursa ya kupanua huduma mbalimbali katika makao makuu hayo ya nchi.

Sabodo alisema kwamba juhudi zake za kuwekeza katika huduma za jamii kama shule, pia ataziendeleza katika mkoa huo kwa kuhakikisha kwamba zinajengwa shule kadhaa za kisasa, ambazo zitamudu mahitaji ya watu wa eneo hilo.

Kwa upande wa huduma ya afya, Sabodo alisema atatumia umaarufu wake kuwashawishi wamiliki wa Hospitali ya kimataifa ya Apollo ya India ili waje nchini wakashirikiane naye kujenga hospitali ya kisasa, ambayo itakuwa inatoa huduma za kisasa mkoani humo.

“Mnaifahamu hospitali ya Apollo ni wawekezaji wakubwa katika huduma za afya, kwa kusukumwa na hatua hii ya Rais nitaongea nao tushirikiane katika kujenga huduma za jamii katika mji huo,” alisema Sabodo.

Pia alisema atawashawishi wawekezaji wengine kutoka nchi za India, Singapore na kwingineko kuja kuwekeza katika mji huo wa Dodoma katika sekta ya viwanda, kuhakikisha kwamba azma ya Rais Magufuli ya kujenga uchumi wa viwanda inatimia.

Sabodo ambaye alisema wazi kuwa utendaji wa Rais Magufuli, umemvutia kutokana na hatua yake ya kupiga vita rushwa, alitangaza kuwa kuanzia sasa hatatoa tena msaada kwa vyama vya upinzani kama ambavyo amefanya miaka ya nyuma kama njia ya kuimarisha demokrasia nchini.

“Huko nyuma nilikuwa nawapa Chadema fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuimarisha demokrasia, sasa natangaza tena kwamba sitawapa tena fedha, niwape za nini wakati Rais aliyeko madarakani anafanya kazi ambayo ndio nilikuwa naipigania?"  alihoji Sabodo.

Sabodo ni mfanyabiashara wa kitanzania mwenye asili ya Kihindi ambaye alizaliwa mkoani Lindi. Katika maisha yake amekuwa anafanya biashara katika nchi za Kenya, Ufaransa, India, Sudan na Zimbabwe.

Pamoja na biashara zake, Sabodo amekuwa anajihusisha kuchangia katika miradi ya maendeleo ya huduma za jamii, uimarishaji wa demokrasia nchini na pia alishiriki kutunisha mfuko wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha bahati nasibu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post