Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, anatarajiwa kufungua kongamano la tano la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linaloandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), litakalofanyikia Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Hassan Mshinda, kongamano hilo la siku tatu litawakutanisha watafiti, wanasayansi, na wabunifu ambapo uwasilishaji wa matokeo ya tafiti mbalimbali na maonesho ya kazi za kisayansi na ubunifu vitakuwa sehemu kubwa ya kongamano hilo.
Aidha, amesema dhima ya kongamano hilo ni “Utafiti Wenye Msukumo wa Kibiashara ni Kichocheo Kuelekea Ukuzaji na Maendeleo ya Viwanda”, ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 katika kuimarisha uchumi wa Taifa unaosukumwa na maendeleo ya viwanda.
Katika kongamano hilo pia, watafiti waliobobea kwenye taaluma mbalimbali, wabunifu, , watunga sera na wadau wengine kutoka sekta za umma na binafsi watajadili kwa kina na kutoa majibu ya namna sayansi, teknolojia na ubunifu vinavyoweza kukuza maendeleo ya viwanda kwa kasi zaidi.
Dkt. Mshinda pia ameeleza kwamba katika kongamano hilo, watafiti wa nchini Afrika ya Kusini na watafiti wa Kitanzania watawasilisha matokeo ya miradi kumi na mitano iliyofadhiliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Afrika ya Kusini, kupitia Mfuko wa Taifa hilo wa Urafiti (NRF) na serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia (MTUSATE), uliopo COSTECH.
“Miradi hiyo ilianza kufadhiliwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili tangu mwaka 2013 na ilipata ufadhili wa miaka miwili ambapo kila nchi ilichangia zaidi ya shilingi milioni mia tano. Matokeo ya tafiti zao kweli yanatupa fursa ya kuwashirikisha watanzania ili wafahamu kinachoendelea katika nyanja ya utafiti,” amesema Dkt. Mshinda .
“Tunawaomba Watanzania kwa ujumla kutembelea tovuti ya Tume ambayo ni www.costech.or.tz kupata taarifa zaidi za kongamano hilo”, ameongeza.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1986, COSTECH ambayo ni mshauri mkuu wa serikali katika matumizi ya sayansi na teknolojia kwa maendeleo ya Taifa, imekuwa ikifadhili tafiti katika maeneo mbalimbali hususani kilimo, afya, ufugaji, uvuvi, TEHAMA, na ubunifu huku ikishirikiana na wadau mbalimbali kama Shirika la Maendeleo la Swideni (Sida), Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID) kupitia Mfuko
wa Ubunifu na Maendeleo ya Watu (HDIF).
Na Hilali Ruhundwa, COSTECH
Social Plugin