Dawa ya Madereva Walevi na Wazembe Hii Hapa...Serikali Yazindua Mkakati Wa Mambo 14 Kupiga Vita Ajali


Serikali yajipanga kupunguza ajali za barabarani kwa kiwango cha takribani asilimia 10 hapa nchini ili kupunguza vifo na majeruhi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Yusuf Hamad Masauni  kuwa baraza la Usalama Barbarani linakerwa sana na kadhia ya ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

“Kukithiri kwa ajali za barabarani kwa siku za hivi karibuni, umewezesha Baraza kuibuka na Mkakati wa Miezi Sita (6) unaolenga katika kukabiliana na ajali za barabarani nchini, mkakati huu ni wa muda mfupi kuanzia mwezi Agosti, 2016  hadi Februari 2017 tutakapokaa na kutathmini matokeo yake”, alisema Masauni.

Masauni amesema ajali za barabarani zimewaacha watoto wakiwa yatima  na kuwafanya akina mama kuwa wajane, hivyo  juhudi za makusudi inabidi zifanywe ili kupunguza kama sio kuondoa kabisa ajali hizo.

Ametaja vyanzo vikuu vya ajali za barabarani nchini kuwa ni pamoja na Makosa ya Kibinadamu, mazingira ya barabara na ubovu wa vyombo vya moto.

Naibu waziri huyo amesema takwimu za ajali barabarani katika miaka mitatu tangu 2012 ajali ziliongezeka toka 23,578 hadi 23, 842 kwa mwaka 2013, vifo vilikuwa 3,969 kwa mwaka huo hadi kufikia 1,043 mwaka 2013.

Vifo hivyo vilipungua hadi kufikia 3,760 mwaka 2014, upungufu huo ulitokana na usimamiaji madhubuti wa Sheria na kanuni za Usalama barabarani pamoja na juhudi zilizofanya na Baraza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Kwa mujibu wa Masauni, Mkakati uliozinduliwa unalenga kudhibiti makosa yanayosababisha madhara makubwa na ambayo husababisha kuongezeka kwa ajali za barabarani.

Ameyataja mambo hayo kuwa  ni:
 1. Udhibiti wa madereva walevi na kuendesha kwa uzembe.

2. Udhibiti wa mwendokasi kwa madereva na wamiliki wa magari; kuwa na madereva wenza

3. Uendeshaji magari bila sifa/leseni ya udereva na bima

4. Udhibiti wa usafirishaji wa abiria kutumia magari madogo yenye muundo wa tairi moja nyuma kwa mfano; Noah, Probox

5. Kudhibiti ajali za pikipiki za magurudumu mawili ‘bodaboda’ na magurudumu matatu

6. Abiria kufunga mikanda ya usalama wanapotumia vyombo vya usafiri

7. Kuyabaini na kuyadhibiti maeneotete na hartarishi ya ajali za barbarani ‘black spots/kilometers’

8. Kuangalia uwezekano wa kufanya marekebisho ya sheria za usalama barabarani.

9. Kuanza kwa mfumo wa nukta ‘point system’ kwenye leseni za udereva.

10. Kutoa mafunzo ya msasa yanayolenga katika kuimarisha utendaji wa askari wa usalama barabarani.

11. Kuhakikisha kuwa waendesha bodaboda wanafikiwa na kupewa mafunzo yaa uhakika juu namna na jinsi ya kuzitumia barabara kwa usalama zaidi.

12. Kudhibiti rushwa na kuwaadhibu watoaji na wapokeaji wa rushwa katika barabara zetu nchini.

13. kuwahusisha wamiliki wa magari ya abiria na ya mizigo, katika kuutekeleza mkakati.

14. Mkakati mwingine waliouweka ni kuwa Dereva ukikamatwa unapelekwa rumande na baadae mahakamani kujibu shitaka litakalokuwa linakukabili.
 Na Jonas Kamaleki-Maelezo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post