Viongozi
wa klabu ya Yanga leo saa nne walikutana katika kikao cha dharura
kufuatia mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji kutangaza kujiuzulu na
kutupilia mbali mpango wake wa kutaka kuikodisha timu hiyo na kuiendesha
kibiashara kwa miaka 10.
Manji
alijiuzulu kwa tuhuma kuwa kuna baaadhi ya viongozi wa Yanga
wamemkashafu na mmoja aliyetuhumiwa kwa kosa hilo ni Katibu Mkuu wa
Baraza la Wazee, Yahya Akilimali.
Maazimio ya Viongozi wa Matawi wa Yanga waliokutana leo katika kikao cha dharura Makao Makuu ya Yanga.
1.
Viongozi hao wamelaani taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari na
Katibu wa Baraza la Wazee, Mzee Akilimali na kuwa haikuwa taarifa
iliyopewa baraka na Yanga.
2.
Viongozi wa Matawi wamemtaka Katibu Mkuu wa Yanga kumfuta uanachama wa
Yanga Yahya Akilimali kwa kosa la kumkashifu mwenyekiti wa Yanga.
3.
Katiba ya Yanga hailitambui Baraza la Wazee badala yake inalitambua
Baraza la Wadhamini, hivyo basi viongozi wa Yanga wamemuomba Katibu Mkuu
wa Yanga kuvunja Baraza la Wazee na wazee hao warudishwe katika matawi
wawe wanachama wa kawaida.
4. Mwanachama yeyote wa Yanga atakayeongea na vyombo vya habari bila idhini ya Yanga, atakuwa amejifuta uanachama wake.
Kwa upande wa Mzee Yahya Akilimali alikuwa na haya ya kusema;-
Sijamtusi
mwenyekiti wangu kwa kusema amekurupuka. Neno hilo ni la kawaida wala
sikuwa na dhamira ya kumtusi mwenyekiti wangu, nawaomba radhi wana-Yanga
kwa kauli zangu. Usiku sijalala nilikosa raha mara baada ya kusikia
Manji kajiuzulu.
Mie naomba tuwe na umoja tatizo letu na mwenyekiti ni kushindwa kutuita wazee kwenye mpango wake wa kuichukua timu.
Sisi
tunampenda na kumuhitaji sana Yusuf lakini tunahitaji aendeleze mfumo
wa zamani alioanza nao wa kujali na kuthamini wazee ili nasi tujisikie
vizuri na klabu yetu.
Nasisitiza
sina chuki na Manji maana kwa mdomo wangu huu nimeshiriki sana kumuweka
madarakani mpaka pale umma wa watanzania wakasema tumevunja katiba.
Ninachotaka alitambue Baraza la Wazee na sisi tukae nae tuzungumze
mstakabali wa klabu yetu.