JPM Kujenga Daraja Kama la Kigamboni la Kuunganisha Busisi na Kigongo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Agosti, 2016 ameanza ziara ya siku mbili katika mikoa ya Geita na Mwanza baada ya kumaliza mapumziko mafupi nyumbani kwake Chato Mkoani Geita. 
 
Jijini Mwanza Rais Magufuli alipokelewa na maelfu ya wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake tangu alipoingia kupitia kivuko cha Busisi – Kigongo na baadaye kupita Usagara, Buhongwa, Mkolani, Nyegezi, Mkuyuni na Igogo ambako pamoja na kuwahakikishia kuwa Serikali yake imejipanga kukabiliana na kero mbalimbali za wananchi na kuwaletea maendeleo, amesitisha agizo la Jiji la Mwanza la kuwataka wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga kutofanya biashara zao katikati ya Jiji ifikapo tarehe 20 Agosti, 2016. 
 
Pamoja na kusitisha agizo hilo, Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kutafuta na kuandaa maeneo ambayo wafanyabiashara hao watayatumia kwa ajili ya kufanyia biashara zao. 
 
“Na mtakapowatafutia maeneo ya biashara wapelekeni sehemu ambazo ni nzuri, msiwapeleke sehemu ambazo hazina biashara, hawa wamachinga wanaendesha maisha yao kwa kutumia biashara hizi” Amesema Rais Magufuli. 
 
 
Aidha, Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mwanza kuwa Serikali imeanza kufanya usanifu na upembuzi yakinifu ikiwa ni maandalizi ya kuanza ujenzi wa daraja kubwa litakalounganisha eneo la Busisi Wilayani Sengerema na Kigongo Wilayani Misungwi ili kuondoa adha ya wananchi kuvuka eneo hilo kwa kutegemea vivuko, na pia itahakikisha inanunua meli moja katika ziwa viktoria kama ilivyoahidi. 
 
 
Kabla ya kuingia Jijini Mwanza Rais Magufuli alihutubia mkutano wa hadhara katika Mji wa Sengerema na pia alizungumza na wananchi wa Sima Wilayani Sengerema na Kasamwa Wilayani Geita ambako aliwahakikishia kuwa Serikali yake itaongeza msukumo katika kutatua tatizo la uhaba wa maji katika maeneo hayo kwa kusambaza maji ya kutoka ziwa Viktoria huku akiwataka viongozi halmashauri husika kutumia rasilimali za halmashauri kutatua tatizo hilo la maji katika maeneo ambayo hayatapitiwa na mradi mkubwa wa maji ya kutoka ziwa Viktoria. 
 
 
Katika hatua nyingine Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa ya Mwanza na Geita kutafakari sababu zilizosababisha kufa kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha NYANZA na viwanda vya kuchambua pamba (Ginneries) ili kupanga namna ya kuvifufua. 
 
Rais Magufuli alitoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kasamwa kilichopo Wilayani Geita na ameahidi kuwa Serikali yake ipo tayari kuunga mkono juhudi za wakulima kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao ikiwemo zao la pamba. 
 
Rais Magufuli atakamilisha ziara yake ya siku mbili leo tarehe 11 Agosti, 2016 kwa kuweka jiwe la msingi katika Daraja la watembea kwa miguu na kuzungumza na wananchi wa Mwanza katika Uwanja wa Furahisha.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza
10 Agosti, 2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post