Kingunge ametoa kauli hii leo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari wakati akiongelea mvutano kati ya Chadema na serikali unaoendelea kwa sasa.
Chadema
kimeingia kwenye mvutano mkubwa na serikali kutokana na dhamira yake ya
kufanya mikutano na maandamano nchi nzima chini ya mwavuli wa Umoja wa
Kupinga Udikteta (Ukuta).
Hivi
karibuni, Rais John Magufuli alisisitiza kutoruhusu maandamano na
mikutano ya kisiasa na kuagiza kuwa, wanaotaka kufanya mikutano wafanye
ndani ya mipaka ya majimbo yao na si vinginevyo jambo ambalo Chadema
wanapinga.
Hali
hiyo imeibua mtikisiko mkubwa nchini huku kada mbalimbali ikiwa ni
pamoja na viongozi wa dini, wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida
wakitaka kupatikana suluhu kabla ya Septemba Mosi, tarehe iliyopangwa
kuanza maandamano na mikutano hiyo.
Kwenye
mkutano wake na wanahabari Kingunge anawalaumu viongozi wastaafu
wakiwemo marais pamoja na mawaziri wakuu kwa kukaa kimwa wakati huu
ambao nchi inatikishwa huku Katiba ya Jamhuri ikisiginwa.
Miongoni
mwa viongozi wanaolalamikiwa kutosikika ama kuchukua hatua zozote ili
kuilinda Katiba ni pamoja na Marais Wastaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi,
Benjamin Mkapa na Aman Abeid Karume (Zanzibar).
Viongozi wengine waliotajwa ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Cleopa Msuya; Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.
“Mzee Mwinyi yupo kimya, Mkapa kimya, Warioba kimya, Cleopa Msuya kimya, Amani Karume kimya,” amesema Kingunge na kuongeza;
“Ukimya
huu unatokana na nini? Hawa wote waliwahi kula viapo vya utii kwa
Katiba. Mimi nahoji, wazee wenzangu vipi mnakuwa kimya? Nawaambia kuwa
mnachofanya si sawa.
“Naomba wazee wote tujitokeze kuhesabiwa katika hili la uvunjifu wa Katiba na sheria.”
Kingunge
ambaye alihamia Chadema akitokea CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
jana kutokana na kutoridhishwa na namna mchakato wa kumpata mgombea
urais kutoka chama hicho amesema, Chadema inatumia haki yake ya
kikatiba.
“Naomba
Rais Magufuli, akubali kuitisha kikao na Chadema ambacho pia wazee
wastaafu watahudhuria, akifanya hivyo hata sisi wazee tutawageukia
Chadema na kuwambia wasitishe mpango wao wa maandamano,” amesema.
Amesema
kwamba, kibaya zaidi Jeshi la Polisi linaandaa bunduki kwa ajili ya
kupambana na raia ambao hawana kitu na kuwa, hali hiyo haipaswi
kuvumiliwa.
Mwanasiasa
huo amesema, Chadema wameamua kutetea haki yao ya kikatiba na kisheria
kwa kufanyaa maandamano kote nchini, na kina wafuasi wengi hivyo si
jambo la kubeza.
“Upande
wa pili, lipo Jeshi la Polisi na watawala ambao wanaahidi kuwakabili.
Kwa bahati mbaya polisi na watawala hawatetei Katiba wala Sheria,” amesema.
Amesema
kuwa, Tanzania kwa sasa inakabiliwa na ombwe la uongozi na kwamba, nchi
imekosa watawala wenye sifa thabiti ya kuongoza taifa.
“Kwa
hakika, tatizo kubwa la sasa la nchi yetu ni ombwe la kiuongozi,
kwasababu kama ni watawala tunao kweli kweli, lakini tunachokosa ni
watawala wenye maarifa ya kiuongozi.
“Inashangaza kuona wazee wastaafu kukaa kimya wakati nchi inakabiliwa na tatizo linaloweza kutuangamiza.
“Upande
mmoja unanoa mapanga, unaanda bunduki kwa ajili ya kuchinja na kuua na
upande wa pili wapo raia tu, tena wasio na silaha zozote.”
Kingunge anasema, wananchi ambao serikali na Jeshi la Polisi wanajiandaa kupambana nao, wanalilia Katiba na sheria zifuatwe.
“Laiti
kama Chadema wangekuwa hawatetei Katiba na sheria, kungekuwa na kila
sababu ya kuwashughulikia, lakini kwa kuwa wanatetea Katiba na sheria,
kuna umuhimu wa kuyapa uzito madai yao,” amesema Kingunge.
Mwanasiasa
huyo amesema kuwa, mvutano wa sasa sio wa Chadema na serikali isipokuwa
ni suala la wananchi wote wa wenye mapenzi mema na taifa lao.
“Hili ni suala la kila mtu anayependa utawala wa Katiba, Sheria na Utawala Bora,” amesema.