Madiwani Saba Waenda Jela Kwa Kumfungia Mkurugenzi Ndani Huko Simiyu...Watalipa Pia Faini ya Shilingi Elfu Moja

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Simiyu imewahukumu kwenda jela miezi sita washitakiwa saba waliokuwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima mkoani humo, kwa kosa la kumfungia ndani aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo.

Mbali na hukumu hiyo, watuhumiwa hao wametakiwa kulipa faini ya Sh 1,000 kila mmoja, huku kifungo hicho kikienda kwa pamoja na kila mmoja kutakiwa kutumikia miezi sita jela.

Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Mlyandingu Cheyo ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Tano Shigilu, Bulikinda Madeleke, Mbuke Mlyandingu, Ntundu Mboyi, Dotto Adam na Nicodemus Ndaki.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 148 ya 2015, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Moses Mafuru, washtakiwa hao walikabiliwa na makosa sita.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkwabi alichukua muda wa saa moja na nusu kusoma maelezo mbalimbali, huku akirejea tofauti za ndani na nje ya nchi ambazo ziliwahi kutolewa na mahakama kwa kesi kama hiyo.

Alieleza kuwa, katika maelezo ya makosa yote sita yanayowakabili washtakiwa yalikuwa yakifanana hali iliyolazimika kuchambuliwa na kubaki makosa matatu.

Alisema kosa la kwanza ni kufanya vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kinyume cha Sheria Namba 5 na 8 Kifungu 385 ya Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambapo washtakiwa walidaiwa kwa pamoja Oktoba 6, 2014 katika ofisi za halmashauri hiyo, walimtishia kwa maneno aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Rogers Shemwelekwa.

Kosa la pili ni kufanya vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kinyume cha Sheria Namba 5 na 8 ya Kifungu 384 cha Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 ambako wanadaiwa kwa pamoja Oktoba 6, 2014 katika ofisi za halmashauri hiyo walimtishia kwa maneno Mwanasheria wa Halmashauri, Engleberth Kalekona.

Kosa la tatu ni vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kinyume na Sheria Namba 5 na 8 Kifungu 385 cha Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambapo wanadaiwa kwa pamoja Oktoba 6, 2014 katika ofisi za halmashauri hiyo walifunga ofisi za halmashauri kwa kufuli.

Pia hakimu huyo, alieleza kuwa mahakama imetupilia mbali utetezi wa upande wa washtakiwa na kubaini utetezi wa upande wa mashtaka ulikuwa na ukweli hali iliyoonesha washtakiwa walitenda kosa kwa nia ya hofu.

Alisema mahakama imewatia hatiani washtakiwa wote kwa makosa yote matatu na kuhukumiwa kifungo cha jela miezi sita kwa kila mmoja na kulipa faini ya Sh 1,000 kila mmoja.
Na Kareny Masasy-Habarileo
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post