Polisi Shinyanga Watibua Ndoa ya Mwanafunzi wa Kidato Cha Kwanza Aliyetolewa Mahari Ng'ombe 16


Bibi na bwana Harusi wakiendelea kufunga ndoa



Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro

******
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na Shirika la Agape Aids Control Programme (AACP) wameendelea kupambana na ndoa katika umri mdogo ambapo jana jioni walifanikiwa kusambaratisha ndoa ya kimila ya mwanafunzi (16) wa shule ya sekondari Usanda wilaya ya Shinyanga.


Binti huyo alikuwa akifungishwa ndoa ya kimila na kijana kutoka kijiji cha Iyombo wilayani Uyui mkoani Tabora, Masumbuko Jineneko (19) aliyekuwa ametoa mahari ya ng’ombe 15,dume watatu na jike 12 na pesa taslimu 100,000/= sawa na ng’ombe 16.


 
Sherehe za harusi zilikuwa zinafanyika kitongoji cha Uswahilini kijiji cha Chabuluba kata ya Usanda wilayani Shinyanga na ndoa hiyo inadaiwa kusimamiwa na baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo diwani wa kata ya Usanda (CCM) na mtendaji wa kijiji cha Shabuluba.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amesema watuhumiwa wote wawili bibi na bwana harusi walikamatwa wakiwa katikati ya sherehe za harusi na kueleza kuwa ni kinyume cha sheria za nchi kwa vile muolewaji ni mwanafunzi wa shule na aliyestahili kuendelea na masomo yake badala ya kuozeshwa.



“Tunaendelea na msako wa kuwatafuta viongozi wanaotuhumiwa kushiriki katika tukio hilo kwani wazazi na bibi harusi,viongozi wa serikali ya kijiji akiwemo diwani wa kata ya Usanda,mtendaji wa kijiji cha Shabuluba na wageni wengine walikimbia na kutokomea kusikojulikana”,alieleza kamanda Muliro.



“Inasemekana kuwa mtuhumiwa tangu achaguliwe mwaka jana kujiunga na shule ya sekondari Usanda hajawahi kuripoti shuleni hapo ambapo kwa maelezo yake anakiri kutokuripoti shuleni na wazazi wake walimkataza kwenda kuripoti shule na inaelezwa kuwa watuhumiwa hawajawahi kukutana kimwili na mtuhumiwa wa kike amepelekwa hospitali ili kupata majibu ya kitaalam kama alishawahi kuingiliwa kimwili”,aliongeza Muliro.


Naye mkurugenzi mtendaji wa shirika la Agape linaloendesha mradi wa kupiga vita na kuzuia ndoa na mimba za utotoni mkoani Shinyanga John Myola alisema alipata taarifa za kuwepo kwa ndoa hiyo kutoka kwa wasiri na kuwasiliana na Jeshi la Polisi ambao alienda nao pamoja katika eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata wahusika wakiwa katikati ya sherehe za ndoa. 

MSIKILIZE HAPA KAMANDA WA POLISI MKOA WA SHINYANGA ACP MULIRO JUMANNE MULIRO AKIZUNGUMZIA TUKIO HILO LA NDOA YA MWANAFUNZI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post