Mbunge wa CHADEMA Godbless Lema Atunishiana Msuli na Mkuu wa Wilaya Mbele ya Waziri

Mbunge wa Arusha Mjini, Goodbless Lema amemvaa Mkuu wa wilaya hiyo, Mrisho Gambo mbele Naibu Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo akidai anaingilia shughuli za halmashauri kinyume na taratibu.

Lema alimtuhumu Gambo kutoheshimu mipaka yake ya kiutawala kwa kuingilia maamuzi ambayo yamejadiliwa kwenye vikao halali vya halmashauri na kupitishwa na ofisi ya mkuu wa mkoa katika kikao cha wakuu wa idara, maofisa tarafa, waratibu wa elimu kata watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Auwsa).

“Nimeona nizungumze hapahapa ili naibu waziri ufahamu hali ilivyo hapa. Kwa mfano, Baraza la Madiwani lililopita ndilo lililopitisha kiwango cha posho kwa madiwani kutoka Sh100,000 hadi Sh120,000, jambo la kushangaza DC ameandika barua Tamisemi na nakala kwa Takukuru ili wachunguze jambo ambalo limeshapata baraka za Tamisemi,” alisema Lema.

Alisema pia amekuwa akiingilia utendaji wa watumishi wa halmashauri kwa kuingilia upangaji wa vibanda vya wafanyabiashara kupitia madalali na kusababisha usumbufu.

Lema aliongeza kuwa Gambo pia amekuwa akitaka uwanja ulionunuliwa na mfanyabiashara urudishwe Jiji wakati kesi imempa uhalali aliyenunua kuchukua eneo hilo.

Hali hiyo ilimfanya naibu waziri kuingilia kati na kuahidi kuzishughulikia changamoto hizo na kumpa nafasi Gambo kujibu madai ya Lema ambayo aliyakanusha, likiwamo la kuingilia utendaji kazi wa mamlaka ya maji.

“Mheshimiwa mbunge nataka ujue mimi ndiyo mkuu wa shughuli za Serikali hapa wilayani, muda wowote nina uwezo wa kuingilia kati mambo ambayo naona hayaendi sawa hata kama yupo katibu tawala na viongozi wengine.

"Rais aliona ninafaa, ndiyo maana akaniteua na sihitaji kujifunza namna ya kuwa mkuu wa wilaya, huu ni mwaka tano,” alisema.

Alisema hakuna siasa kwenye maendeleo ya wananchi na kumtaka mbunge atambue kuwa kuhudumia wananchi hakuhitaji maamuzi ya Baraza la Madiwani pekee, kwani kumekuwa na tabia ya kutumia fedha za halmashauri vibaya kulipana posho ambazo hazipo kwa mujibu sheria na kanuni.

Alisema alilazimika kutaka viongozi walio chini yake kupitia hukumu iliyompa mfanyabiashara eneo la Kilombero kama ni halali na kushangazwa na Lema kupinga.

Akizungumzia suala hilo, Jaffo alimtaka Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega kushughulikia changamoto hizo akisema muda wa siasa umepita na wananchi wanahitaji maendeleo.

Pia, alisema Serikali ipo mbioni kuwahamisha watumishi wa halmashauri ya jiji wanaofanya kazi kwa mazoea na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Athuman Kihamia kusimamia wafanyakazi wanaofanya kazi kwa mazoea huku wananchi wakipata shida.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post