Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Mchungaji wa Kanisa Aliyehifadhi Meno ya Tembo Kanisani Katavi Ahukumiwa Kifungo Jela Miaka 20

Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi imemuhukumu Mchungaji wa Kanisa la Moroviani Usevya Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi Godwel Siame kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukamatwa na nyara za Serikali meno ya Tembo yenye thamani ya Tsh Milioni 90 akiwa ameyahifadhi ndani ya kanisa .

Hukumu hiyo iliyovutia hisia za watu wengi wa Manispaa ya Mpanda na Mkoa wa Katavi ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Chiganga Ntengwa baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka na utetezi .

Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliongozwa na mwanasheria mfawidhi wa serikali wa mkoa wa Katavi Acheres Mliso na mshtakiwa Mchungaji Siame alitetewa na wakili Patrick Mwakyusa ambapo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi sita na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi wanne .

Awali katika kesi hiyo mwendesha mashtaka wa serikali Acheres Mliso alidai kuwa mshtakiwa Mchungaji Godwel Siame alitenda kosa hilo  Mei 5 mwaka huu katika Kijiji cha Usevya Wilaya ya Mlele .

Siku hiyo ya tukio mshtakiwa ambaye alikuwa ni mchungaji wa Kanisa la Moroviani Usevya alikamatwa na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi na Askari wa jeshi la polisi akiwa na nyara za serikali Meno ya Tembo vipande 11 vyenye uzito wa kilo 20 yenye thamani ya Tsh Milioni 90 akiwa ameyahifadhi ndani ya Kanisa la Moroviani Usevya alikuwa akiliongoza kama mchungaji wa Kanisa hilo.

Ilidaiwa kuwa aSkari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi pamoja na Askari Polisi walipata taarifa kutoka kwa Raia wema wa Kijiji cha Usevya kuwa mchungaji Godwel Siame anajishughulisha na biashara ya meno ya Tembo na amekuwa akiyahifadhi ndani ya Kanisa analoliongoza .

Mwendesha mashitaka huyo wa Serikali alidai kuwa baada ya taarifa hizo polisi na Askari Tanapa walifika katika eneo hilo siku hiyo na ndipo walipoweza kufanikiwa kukamata meno yaTembo vipande 11 yenye thamani ya Tsh Milioni 90 yakiwa yamehifadhiwa ndani ya Kanisa Moroviani Usevya.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Chiganga Ntengwa kabla ya kusoma hukumu aliiambia Mahakama kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo wa pande zote mbili za mashitaka na utetezi Mahakama pasipo shaka yoyote imeona mshitakiwa anayo hatia hivyo kw a misingi hiyo inampa nafasi mshitakiwa kama anayosababu yoyote ya msingi ya kuishawishi Mahakama impunguzie adhabu .

Katika utetezi wake mchungaji Siame aliliomba Mahakama imwachie huru kwani yeye hakujua kama ndani ya Kanisa lake kuna Meno ya Tembo yamehifadhiwa humo na ndio maana walipomkamata wakati akiwa nyumbani kwake hakuwa na shaka yoyote ile .

Utetezi huo ulipingwa vikali na Mwendesha Mashitaka Mwanashria Mfawidhi wa Serikali wa Mkoa wa Katavi Acheres Mliso ambae aliiomba Mahakama ipatie adhabu kali mshitakiwa ili iwe fundisho kwa viongozi wenzake wa Dini ambao wanatabia kama hiyo .

Hakimu Chiganga baada ya kusikia maombi ya mshitakiwa aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa Mchungaji Godwel Siame amapatikana na hatia ya kifungu cha sheria N0 86 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha sheria ya uhifadhi wa wanyama pori N0 5 ya mwaka 2009 na kifungu cha sheria N0 57 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya uhujumu uchumi sura N0 200 marejeo ya mwka 2000.

Hivyo Mahakama imemuhukumu Mchungaji Godwel Siame kutumikia kifungo cha miaka ishirini jela kuanzia jana na kama haja ridhika na uamuzi huo anaruhusiwa kuomba rufaa ndani ya siku 30 kuanzia jana.
 
Na  Walter   Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi 
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com