MCT YAMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KUPAMBANA NA RUSHWA NA UBADHIRIFU




BARAZA la Habari Tanzania (MCT) limeipongeza serikali ya Rais John Magufuli kwa jitihada zake za kupambana na rushwa pamoja na ubadhirifu na kusema inapaswa kuungwa mkono na kila mmoja na pia vyombo vya habari.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alitoa pongezi hizo jana wakati wa Mkutano Mkuu wa 18 wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mukajanga alisema kwa kuwa vyombo vya habari ni namba moja katika kupambana na rushwa, wanaiomba serikali itafute suluhu pale vinapokosea badala ya kuvifungia.

“Midhali serikali inajua sheria zilizopo zinahitaji marekebisho, tupunguze kuzitumia kwa sababu hazitupeleki mbele, bali zinaturudisha nyuma,” alisema Mukajanga.

Alisema hivi sasa Kamati ya Maadili ya Baraza hilo ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Juxon Mlay inaendelea kukusanya ushahidi wa kutosha ili waende kuzungumza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuhusu mgogoro huo wa kuvifungia vyombo vya habari.

Vyombo vya habari vilivyofungiwa na serikali hivi karibuni ni gazeti la Mseto na vituo vya redio vya Magic FM na Radio Five. Naye Rais wa baraza hilo, Jaji Thomas Mihayo alivitaka vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari visiogope kutumia haki yao ya msingi pale inapotokea wanavunjiwa uhuru wao wa kujieleza kwa sababu mahakama ni sehemu sahihi ya kudai haki kamili.

“Watanzania wengi hawapendi kutumia vyanzo sahihi vya kuweza kupata haki yao. Waandishi wa habari mnapotaka kupata haki yenu nendeni mahakamani kwa sababu ni chombo cha pekee kinachoweza kutoa haki ya kweli," alisema Jaji Mihayo.

Mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti la MwanaHalisi, Said Kubenea alisema kuna tatizo kwa waandishi wa habari kuwa wavivu katika kutafuta haki mahakamani, pengine ni kutokana na mchakato mrefu.

Aliiomba MCT kuwa mstari wa mbele katika kuzisimamia kesi hizo mahakamani, kwa kuwa kwa kufanya hivyo kutaipa kesi hizo nguvu.

“Ni rai yangu MCT, lisimame katika kutetea waandishi na vyombo vya habari," alisema Kubenea. Katika hilo, Mukajanga alisema hilo ni jukumu lao wamelipokea hivyo watatenga fedha kwa ajili ya kusaidia uhuru wa habari nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post