Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amepiga marufuku mikutano ya Operesheni Ukuta iliyotangazwa kuratibiwa na Chadema kuanzia Septemba Mosi.
Akizungumza katika kikao cha kazi kilichoshirikisha kamati ya ulinzi na usalama mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri, Makalla alitangaza kupiga marufuku mkutano wowote utakaofanyika chini ya utaratibu unaoitwa Operesheni Ukuta.
“Bila shaka wananchi wa Mbeya wanataka amani na kazi, hivyo ni marufuku kufanyika mkutano wowote wa kisiasa unaoandaliwa kwa kushirikiana na watu wengine kutoka nje ya mkoa,” alisema Makalla aliyewahi kuwa mbunge na mweka hazina wa CCM.
Alifafanua kuwa wabunge na madiwani akiwamo Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) wa Chadema wanaweza kufanya mikutano yao bila wasiwasi katika maeneo yao.
Makalla alisema vyombo vimewekwa tayari kuwashughulikia kwa nguvu zote watakaokaidi maagizo yanayotolewa na kutoa mwito kwa vijana wa mkoa huo kuwafichua watu wenye njama zozote zikiwamo za kuwahamasisha kufanya maandamano au mikutano.
Polisi yadai kukamata vijana
Wakati Makalla akipiga marufuku Operesheni Ukuta, Polisi mkoani Mbeya wameeleza kuwakamata vijana wawili wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema kwa tuhuma za kuandaa na kusambaza ujumbe wa sauti wenye kauli za kutaka ofisi za CCM zichomwe moto.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Dhahir Kidavashari alidai kwamba vijana hao waliandaa na kusambaza ujumbe huo Julai 29 ukiwataka vijana wenzao ambao ni wanachama wa chama hicho kwenda kuchoma moto ofisi za CCM mahali walipo.
Kidavashari alidai kwamba ujumbe huo unahamasisha vijana kufanya uhalifu huo wakati wowote kabla ya Septemba Mosi na baada ya hapo ilimradi nchi iwe kwenye machafuko.
“Baada ya kufuatiliwa na kumkamata, mtuhumiwa wa kwanza alipekuliwa na kukutwa na simu ambazo zilitumika kusambaza ujumbe huo.Pia kupitia mtuhumiwa huyo tulifanikiwa kumpata mtuhumiwa mwingine.”
Social Plugin