Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni, Mh Ally Hapi leo ametengua uteuzi wa aliyekuwa
Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Delila
Mushi kwa kosa la kupandisha bei ya baadhi ya huduma kinyume cha
taratibu na sheria.
Mushi
amedaiwa kupandisha bei ya huduma hizo baada ya kukaa kikao cha
hospitali pasipo kuipeleka hoja ya kupandisha bei katika kikao cha Idara
ya Manispaa na huduma za jamii.
Taratibu
alizotakiwa kufuata Mushi ni kuipeleka hoja hiyo Manispaa, ambapo
ingejadiliwa kwenye kikao cha huduma za jamii kisha baraza la madiwani
kuipitia na kuitolea maamuzi jambo ambalo hakulifanya badala yake
alipandisha bei pasipo kupitia taratibu hizo.
Bei
ya huduma zilizopandishwa ni pamoja na bei ya kadi ambapo wagonjwa
waliofika katika hospitali hiyo bila ya barua ya rufaa kutoka vituo vya
afya na zahanati zilizo karibu nao, walitakiwa kulipa sh 10,000 badala
ya 6,000.
“Hakuna
jambo baya kama kiongozi kufanya maamuzi pasipo kufuata utaratibu
halafu maamuzi hayo yakaathiri wananchi wanyonge, mkurugenzi nakuagiza
hiyo bei ya kadi irudi kama ilivyokuwa awali, huwezi mlipisha mgonjwa
kiasi kikubwa cha fedha huku huduma unazotoa haziendani na bei hiyo, ” amesema Hapi.
“Hakuna
sababu ya anayekaimu nafasi ya mganga mkuu kwa sasa kubaki na wadhifa
huo wakati haumtoshi, atatafutwa mwIngine kuja kuwa mganga Mkuu, ” amesema.
Kwa sasa ameteuliwa Dkt. Daniel Nkungu kukaimu kwa muda wadhifa huo hadi atakapoteuliwa mganga mwingine kushika wadhifa huo.
Hata
hivyo, Baada ya Hapi kutoa agizo la kutenguliwa uteuzi wa Dkt. Mushi na
kuamuru Wagonjwa kulipa bei ya kadi ya awali, baadhi ya wahudumu wa
mapokezi waligoma kutoa huduma kwa madai kuwa mifumo ya utoaji risiti
imeharibika.
Mariam Hamisi Sahabani mkazi wa Kinondoni, alifafanua jinsi wahudumu hao walivyogoma baada ya mkuu wa wilaya kuondoka.
“Baada
ya Mheshimiwa kuondoka wamegoma kutoa huduma kwa kigezo kuwa mashine
ilikuwa mbovu, inawezekanaje? Mbona wakati tunalipa 10,000 mashine
zilifanya kazi, iweje sasa zisifanye? ” alihoji.
Kufuatia
malalamiko hayo yaliyotolewa na wananchi waliokuwepo kwenye hospitali
hiyo, Mganga mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Aziz Msuya alisema
atawasimamisha kazi waliogoma kutoa huduma kwa kuwa walikuwa na lengo la
kupinga kauli ya serikali.
“Naagiza huduma ianze kutolewa kuanzia sasa, na watakaogoma kutoa huduma nitawasimamisha kazi kuanzia kesho, ” amesema Msuya.