Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amewasihi wadau wote wa siasa wenye mipango ya kufanya maandamano na mikutano wasubiri kwanza yafanyike mazungumzo ili kumaliza mvutano uliopo kwa njia ya amani.
Akiongea jana na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisini kwake Jaji Mutungi amesema yeye kama mlezi wa vyama vya siasa nchini, anaamini kuwa pale panapokuwa na sintofahamu njia pekee ya kupata ufumbuzi ni kukaa pamoja na kujadiliana.
Aidha, Jaji Mutungi ambaye pia ni Mratibu wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, amesema baraza litakaa vikao vyake tarehe 29 na 30 mwezi huu, ambapo pia wataalikwa wageni ambao watakuwa na mchango mkubwa katika masuala makubwa yaliyojitokeza na yoliyoleta sintofahamu iliyopo hivi sasa.
Jitihada hizo za Baraza la Vyama vya Siasa nchini, zinazoungana na jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini katika kuepusha mvutano uliotokana na maandamano na mikutano yaliyotangazwa na baadhi ya vyama kufanyika nchi nzima.