Baraza Kuu la Uongozi la Chama
cha Wananchi (CUF) limemteua Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti wa kamati
ya muda ya uongozi hadi utakapoitishwa mkutano mkuu maalumu mwingine
baada ya ule wa awali kuvunjika.
Mtatiro amekubali uteuzi huo na kwamba hawezi kukwepa
majukumu hayo muhimu.
Baraza hilo lililoketi katika kikao chake cha
dharura juzi Jumapili mjini Unguja, liliamua pia kusitisha uanachama wa
baadhi ya watendaji wake waandamizi, kutoa karipio kali na kuwafukuza
baadhi yao.
Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za makao makuu ya
chama hicho, Vuga kilihudhuriwa na wajumbe 47 kati ya 60 na kiliongozwa
na Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali.
Akitangaza maazimio ya kikao
hicho jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui
alisema katika kutekeleza jukumu hilo, Mtatiro atasaidiana na Katani
Mohamed Katani na Severina Mwijage.
“Maamuzi hayo ni kwa mujibu wa
katiba ya CUF kifungu Na.101 na 118, vinavyolipa mamlaka baraza
kutekeleza hatua hiyo.”
Mazrui alisema baraza hilo lilimteua John
Bashange kukaimu nafsi ya naibu katibu mkuu wa CUF – Tanzania Bara na
Mbaralah Maharangande kukaimu nafasi ya naibu mkurugenzi wa habari,
uenezi na uhusiano kwa umma.
Nafasi zilizojazwa ziliachwa wazi na
Profesa Ibrahim Lipumba, Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya ambao baraza
hilo la dharura lilitangaza kuwasitisha uongozi na uanachama wao.
“Hatua
ya kuitisha baraza la dharura sambamba na maamuzi hayo ilikuja baada ya
kushindwa kupata uongozi wa juu wa chama kufuatia kuvunjika na
kushindwa kukamilika kwa mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa Agosti 21
uliofanyika jijini Dar es Salaam,” alisema.
Alisema kuwa baraza liliamua
kusitisha uanachama wa Sakaya kwa kushindwa kutekeleza kifungu cha
katiba ya CUF, Na. 122 na kwamba licha ya barua aliyotumiwa kumtaka
ahudhurie kikao hicho, hakufika bila ya taarifa yoyote ya msingi.
Mazrui
alisema katika baraza hilo, ilielezwa kuwa Sakaya alidai kuzuiliwa na
wazee wa CUF wa Dar es Salaam kwa madai kuwa hicho hakikuwa kikao
halali.
Wengine ambao uanachama wao umesitishwa ni Ashura Mustafa,
Mohamed Mnyaa, Kapasha Kapasha, Haroub Shaim, Omar Masoud na Thomas
Malima.
Baraza hilo la CUF lilitangaza kumfukuza uanachama wa chama
hicho, Shashu Lugeye, baada ya kumsikiliza na kutoridhishwa na maelezo
yake.
Wanachama waliopewa karipio kali ni Rukia Kassim Mohamed na Othman Mohamed.
“Chama
kimechukua maamuzi haya kuonyesha dhamira ya dhati na matumaini ya
umma wa Watanzania kwamba CUF ndiyo pekee iliyobeba dhana ya
mabadiliko,” alisema Mazrui.
Taarifa kutoka ndani ya Baraza hilo
ziliarifu sababu tatu za kuchukua hatua hiyo kuwa ni hasara ya Sh600
milioni kiliyoingia kwa mkutano uliovunjika; njama ovu zilizodaiwa
kutekelezwa na baadhi ya watendaji wao; na jaribio la kuchafua taswira
ya chama hicho.
Mazrui alisema mkutano mkuu maalumu, kabla ya ule wa
kawaida wa mwaka 2018 kwa mujibu wa Katiba, utafanyika pale chama hicho
kitakapopata uwezo wa kifedha.
Akiandika katika mtandao wake wa Facebok, Mtatiro alisema,
“Nimepokea majukumu niliyokabidhiwa na Baraza Kuu la chama changu.
Siwezi kuepuka majukumu haya muhimu kwa wakati huu ambapo chama
kinahitaji mchango wangu. Niko imara sana, natambua nimepewa majukumu
wakati gani na nianze na mguu upi kwenda mbele”.