Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Mwalimu Aliyedaiwa Kufanya Mapenzi na Wanafunzi Auawa Kwa Kipigo cha Wananchi Huko Simiyu


MWALIMU Daniel Msalika (42) wa shule ya msingi Nyasosi, wilayani Bariadi, mkoa wa Simiyu amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikokuwa amelazwa akitibiwa majeraha.

Majeraha hayo yalitokana na kushambuliwa na baadhi ya wananchi kwa madai ya kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wa kike wa shule hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga aliwaeleza waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa mwalimu huyo alifariki dunia Julai 31 mwaka huu saa nane usiku.

Kamanda Lyanga alisema kuwa siku ya tukio Julai 27 mwaka huu saa 6.30 usiku, wananchi hao ambao idadi yao haijafahamika, walivamia nyumba ya mwalimu huyo baada ya kupata taarifa kuwa kuna mwanafunzi ambaye amelala nyumbani kwake, jambo ambalo halikuwa la kweli.

“Wananchi hao walipata taarifa ya kuwa nyumbani kwa mwalimu kuna mwanafunzi ambaye amelala humo hivyo walimvamia kwa kuvunja mlango na kuanza kumshambulia kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi na kumsababishia majeraha makubwa sehemu za kichwani na usoni lakini binti waliyemkuta kwake ni mwenye umri wa miaka 18 na siyo mwanafunzi,” alisema.

Alisema kuwa baada ya uvamizi huo, mwalimu huyo alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Isanga kupatiwa matibabu, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, lakini alifariki dunia.

Kamanda alisema kifo chake, kimesababishwa na majeraha ya kushambuliwa huku tuhuma dhidi yake zikiwa si za kweli.

Alitoa mwito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi huku wakisisitiza kuwa wote watakaobainika kusababisha kifo hicho, sheria itachukua mkondo wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com