Mbio za Mwenge wa Uhuru zimetua Kanda ya ziwa huku zikizua sintofahamu kwa watumishi wa umma waliotakiwa kutokukosa mkesha wake ili kukwepa rungu la Mamlaka za kinidhamu dhidi yao.
Taarifa kutoka wilayani Sengerema zilieleza kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ameagiza watumishi wote wa wilaya hiyo kuhakikisha wanahudhuria mkesha huo na kwamba daftari la mahudhurio litaitishwa majira ya saa 6 usiku, saa 9 usiku na saaa 12 usiku.
Hayo yamebainishwa katika Tangazo rasmi lililosainiwa na Msangi M.A kwa niaba ya Mkurugenzi, Magessa Boniface.
Aidha, katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, imeelezwa kuwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari waliitwa katika kikao na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mary Tesha ambaye aliwaeleza kuwa ambaye hatahudhuria mkesha huo atakumbwa na adhabu ikiwa ni pamoja na kushushwa vyeo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alipotafutwa, alikana kuwaeleza walimu hao kuwa wangeshushwa vyeo kama wasingehudhuria ingawa alikiri kuwa alikutana nao.
“Sijasema hayo, nilichosema ni kuwa Mwenge ni jukumu letu watumishi tunapaswa kushiriki. Hao walimu ni wajumbe wa Kamati za Mbio za Mwenge hivyo wanapaswa kushiriki. Hilo la kufukuza, kuwawajibisha hapana,” alisema Tesha.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Nyamagana, Asha Juma alisema kuwa ingawa amesikia kuwepo kwa maagizo hayo, hajapata malalamiko kutoka kwa walimu.
“Najua wanahamasisha watumishi waende, lakini nadhani wangetafuta njia nyingine ya kuwahamasisha sio vitisho,” alisema Katibu huyo wa CWT.