Muimbaji mkongwe wa muziki wa Taarab nchini, Bi. Shakila Said, atazikwa Jumamosi hii. Bi. Shakila alifariki ghafla jana Ijumaa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa shirikisho la muziki Tanzania, Addo November, muimbaji huyo alifariki ghafla mara baada ya kumaliza kuswali nyumbani kwake, Mbagala Charambe jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mwanae, Shani, mama yake alianguka na kupoteza maisha na kwamba hakuwa akiumwa. Mazishi yake yanafanyika kwake Mbagala.
Bi Shakila aliwahi kuwika na nyimbo kadhaa ukiwemo ule maarufu, MACHO YANALIA MOYO UNACHEKA aliouimba akiwa na bendi ya JKT miaka ya 90.
Mwaka 1960, aliolewa akiwa na umri wa miaka 11 tu na kuachana akiwa na mtoto mmoja kabla ya kuolewa tena na mwanaume aliyedumu naye kwa miaka 18 na kuzaa naye watoto watano kabla ya mumewe kufariki mwaka 1975.
Alikuja kuolewa tena na mwanaume mwingine aliyezaa naye watoto watano kabla ya kuja kuolewa tena mara ya nne na mwanaume aliyezaa naye watoto wawili.
Alipokuwa na mimba ya mtoto wake wa mwisho, Shani, mume wake alimwacha. Shani alizaliwa mwaka 1993 na hapo ndipo alidai alichukia wanaume na kuamua kuishi mwenyewe.
Pamoja na kustaafu kazi JKT, Shakila aliendelea kufanya muziki na miaka miwili iliyopita alikuwa akirekodi album yake Mama na Mwana ambayo ingekuwa na nyimbo nane.
Social Plugin