Ndani ya ukumbi baada ya kutokea vurugu
Prof. Lipumba akiwa ukumbini
Mkutano Mkuu wa dharura wa Chama cha Wananchi CUF umevunjika baada ya kundi la wafuasi wa chama hicho kuvamia na kufanikiwa kuzima mchakato wa kupiga kura kumchagua mwenyekiti mpya wakishinikiza aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba aruhusiwe kurejea katika wadhifa huo.
Wafuasi hao wameingia ukumbini wakati wajumbe zaidi ya 700 wa mkutano huo wakijiandaa kupiga kura usiku huu kumchagua mwenyekiti, jambo lililozua vurugu zilizoambatana na uvunjaji wa viti na meza.
Kufuatia hali hiyo, mwenyekiti wa mkutano huo, Julius Mtatiro amelazimika kuahirisha uchaguzi mpaka utakapotangazwa tena.
Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu wadhifa huo Agosti mwaka jana baada ya kutofautiana na vyama vinavyounda Ukawa kwa kumpokea Edward Lowassa, alitoka nje ya ukumbi wa Blue Pearl jijini Dar es salaam ulikofanyika mkutano huo, huku akisindikizwa na vijana waliokuwa wakiimba nyimbo za kumsifu.
Inaelezwa kuwa Maalim Seif, Julius Mtatiro wamekacha na kukimbia mkutano huo maalum wa CUF baada ya hoja yao ya uchaguzi wa mwenyekiti kukataliwa na wajumbe na kumtaka prof. Lipumba aendelee.
Habari zinasema kuwa jaribio la kumzuia Lipumba asiingie ukumbini lilikwama na wanachama kumuingiza kwa nguvu ndipo kikao kikaahirishwa huku prof. Lipumba akiendelea kubaki ukumbini.
Mpaka sasa seif na mtatiro hawajulikani walipo, inasemekana wameenda kuchukua maelekezo.
Profesa Lipumba aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani kuanzia 1995 hadi mwaka jana, aliachia ngazi kwa kile alichodai kupinga uamuzi wa viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Baada ya profesa huyo wa uchumi aliyegombea urais mara nne kujiweka kando, CUF iliunda kamati ya watu watatu chini ya uenyekiti wa Twaha Taslima, kukiongoza chama hicho hadi hapo utakapofanyika uchaguzi mwingine wa viongozi.
Waliowahi kuwa wenyeviti wa chama hicho ni Profesa Lipumba, Musobi Mageni na James Mapalala.
Wanaogombea uenyekiti ni Abdul Omary Zowo , James Mahangi , Joseph Rhobi , Juma Nkumbi , Salum Barwany, Selemani Khatibu, Zuberi Kuchauka, Riziki Mngwali na Twaha Taslima.
Wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti ni Dk Juma Ameir Muchi, Juma Duni Haji, Mussa Haji Kombo na Salim Abdallah Bimani.
Chama hicho kilionekana kama kitayumba baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu, lakini kilivuka kigingi hicho na katika Uchaguzi Mkuu uliopita kilishinda viti 10 vya ubunge Tanzania Bara, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kilipoanzishwa.
Hata hivyo, chama hicho, kwa upande wa Zanzibar hakikupata nafasi ya wabunge wala uwakilishi baada ya kususia uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20.
Uchaguzi huo wa marudio ulifanyika baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Taarifa rasmi tutawaletea hivi punde,endelea kutembelea Malunde1 blog