SIKU
mbili baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuahidi kufanyika maridhiano
kati ya uongozi wa Bunge na wabunge wa upinzani katika kikao kijacho
kinachotarajiwa kuanza Septemba 6, mwaka huu, Naibu Spika, Dk. Tulia
Ackson amesema hataki kuwasikia wabunge wa upinzani wala kuwawaza.
Kauli
hiyo ya Naibu Spika huenda ikazidi kutonesha kidonda hasa baada ya
Bunge la Bajeti lililofanyika Mei mwaka huu kuacha majeraha kutokana na
wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
kususia vikao vyote vilivyoendeshwa na kiongozi huyo.
Juzi
wakati akihojiwa kupitia kipindi cha Funguka kinachorushwa na Kituo cha
Luninga cha Azam, Spika Ndugai, alisema anatafuta mbinu ya kuweka sawa
mambo hayo kwa kufanya maridhiano ikiwemo kushirisha maspika wastaafu.
Akizungumza
na gazeti la Mtanzania juzi katika mahojiano maalumu ofisini kwake
jijini Dar es Salaam, Dk. Tulia alisema hapendi kuwawazia wabunge hao wa
upinzani.
“Kwa kuwa Spika yeye kazungumza siwezi kucomment chochote kwa sababu sipendi kuwawazia wabunge hao,”alisema.
Alipoulizwa
kwamba ni kwanini migogoro ilizidi wakati yeye akiwa anaendesha vikao,
alisema alichokuwa anafuata ni kanuni na kwamba malalamiko hayawezi
kukosekana.
“Nashangaa
wengine wanasema kuendesha vikao ni mpaka uwe na uzoefu…unajua zile
kanuni hata ukipewa uendeshe wewe ukishazielewa hazihitaji uzoefu
wowote. Kulalamika kuwa nawapendelea ni jambo la kawaida.
“Kwa
mfano siku iliyotokea vurugu wakati wabunge wa upinzani wanadai
kutorushwa matangazo ya Bunge live, aliyekuwepo kwenye kiti alikuwa ni
mwenyekiti ambaye ni mzoefu wa siku nyingi na ni yeye aliyepeleka majina
yao kwenye Kamati ya Maadili, sasa sidhani kama hiyo ni hoja,”alisema Dk. Tulia
Alieleza
kushangazwa kwa kitendo cha wabunge wa upinzani katika barua yao
waliyomwandikia Spika kwamba hawana imani naye, huku akihusishwa na
fedha zilizorejeshwa serikalini.
“Katika
ile barua walieleza sababu nyingine kuwa hawana imani na mimi,
wakanihusisha na zile Shilingi bilioni 6 zilizorejeshwa serikalini
wakati sheria na utaratibu upo wazi kwa sababu Spika au Naibu Spika
hauhisiki na masuala ya fedha bali anayehusika ni Katibu wa Bunge.
“Kwa
hiyo ni jambo la kushangaza kwamba Naibu Spika karudisha fedha, mimi si
mshika mafungu lakini pia ni namna watu walivyopokea huwezi kuwazuia
wanavyokuwazia,” alisema.
Akizungumzia
kauli ya Spika Ndugai kwamba kwa kuwa Bunge la 11 lina wabunge wapya
wengi na kwamba kuwaongoza kunahitaji uvumilivu mkubwa alisema: “Nisingependa
kuongelea kauli ya Spika…lakini uvumilivu wa mtu kutakiwa akae hadi
mara 11 halafu ameendelea kusimama ni uvumilivu gani huo?,” alihoji.
Pamoja
na mambo mengine alisema wakati wabunge wanawake wa Ukawa walipojitoa
kwenye Chama cha Wabunge Wanawake (TWPG), alitukanwa tusi kubwa lakini
alinyamaza.
Mei
5, mwaka huu wakati akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato
na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria, Mbunge wa Ulanga Mashariki,
Gudluck Mlinga (CCM), alidai kuwa ili kuwa mbunge wa viti maalumu
Chadema lazima uwe ‘baby’ wa mtu.
“Laiti
ungeona Hansard tusi walilonitukana siku ile, actually Mlinga
hajatukana lakini ulisikia nikilalamika mahali kwamba nimetukanwa? wao
wanaongee vibaya…watukane, mimi bado ni kiongozi wao na siwezi kuanza
kuwakasirikia itakuwa sasa nashindwa kuwaongoza mimi ni kama mzazi wao,” alisema Dk. Tulia.
Alisema
kitendo cha watu kudai kwamba anafanya upendeleo bungeni ni changamoto
ya kawaida, kwa sababu hata katika mabunge ya Jumuiya ya Madola
malalamiko ya aina hiyo yapo.
“Pale
bungeni wako wabunge 389, hawa ni wengi sana wote hawawezi kupata
nafasi ya kuongea. Kwa mfano uliomba nafasi jana ukapewa ukaomba leo,
hata ukisimama mara 11 katika hali ya kawaida huwezi kupewa kwa sababu
wako wengi ambao hawajachangia.
“Kama kiongozi naona ni sehemu mojawapo ya kusimamia jamii ni changamoto na itaendelea kuwepo kwa miaka mitano,”alisema Dk. Tulia.
Social Plugin