Picha : Mgodi wa Williamson Diamonds Ltd "Mgodi wa Mwadui" Waipiga Tafu ya Madawati Shule ya Msingi Bugweto Shinyanga

Hapa ni katika shule ya Mwadui Shule ya Msingi iliyopo katika Mgodi wa Williamson Diamonds Limited maarufu Mgodi wa Mwadui uliopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.


Agosti 02,2016 Mgodi wa Williamson Diamonds ulikabidhi msaada wa madawati 25 yenye thamani ya shilingi 2,500,000/= kwa ajili ya shule ya msingi Bugweto iliyopo katika kata ya Ibadakuli katika manispaa ya Shinyanga.

Msaada huo wa madawati 25 umekuja siku chache tu baada ya mgodi huo kutoa madawati 1,000 katika wilaya ya Kishapu ikiwa ni katika jitihada za kutii agizo la rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa wanafunzi wote wanakaa katika madawati shuleni.


Akikabidhi msaada huo, Meneja Mahusiano wa mgodi huo Joseph Kaasa alisema wameamua kutoa msaada huo baada ya kupokea ombi la diwani wa viti maalumu katika manispaa ya Shinyanga Zuhura Waziri (CCM) anayetoka tarafa ya Ibadakuli kuhusu mahitaji ya shule hiyo iliyopo katika kata ya Ibadakuli.


“Ombi hili limekuja katika kipindi ambacho hatuna pesa,lakini tumeona ni vyema tutoe msaada huu ili kuunga mkono jitihada za rais John Pombe Magufuli katika kuhakikisha wanafunzi wanakaa kwenye madawati,tuko tayari kuendelea kutoa misaada katika shule ili kupunguza matatizo katika shule zetu”,alisema Kaasa.


Alisema katika vijiji vyote 14 vinavyozungukwa na mgodi huo hakuna upungufu wa madawati,madarasa wala nyumba za walimu na wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ya kijamii ikiwemo huduma ya maji na afya.


Diwani wa Viti Maalum katika manispaa ya Shinyanga anayetoka tarafa ya Ibadakuli ,Zuhura Waziri (CCM) aliyekuwa ameambatana na diwani wa kata ya Ibadakuli Msabila Mabula ilipo shule hiyo aliushukuru mgodi huo kwa kuisaidia shule hiyo huku akiuomba mgodi huo kuendelea kuzisaidia shule za manispaa ya Shinyanga kwani bado zina changamoto lukuki.

Akipokea msaada huo wa madawati, mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya msingi Bugweto ,Suzana Mabula pamoja na kupokea msaada huo wa madawati,alipaza kuwa shule yake yenye jumla ya wanafunzi 585 na walimu 16 inakabiliwa na uchakavu wa majengo ambayo hayana sakafu na yana nyufa zinazotishia usalama wa wanafunzi wao.


Mwalimu Mabula alisema shule hiyo pia haina nyumba za walimu,ofisi ya walimu ambapo walimu wanalazimika kutumia darasa moja kama ofisi wakitumia madawati ya wanafunzi kama meza na viti vya ofisi kutokana na uhaba wa meza na viti vya walimu.
Kulia ni Meneja Mahusiano wa mgodi wa Williamson Diamonds Limited Joseph Kaasa akikabidhi madawati kwa Diwani wa Viti Maalum manispaa ya Shinyanga anayetoka tarafa ya Ibadakuli mheshimiwa Zuhura Waziri (CCM) na diwani wa kata ya Ibadakuli Msabila Mabula (kushoto).
Kulia ni Meneja Mahusiano wa mgodi huo Joseph Kaasa akiwa amekaa kwenye moja ya madawati yaliyotolewa na mgodi wa Mwadui .Katikati ni Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Shinyanga Zuhura Waziri (CCM) na diwani wa kata ya Ibadakuli Msabila Mabula (kushoto).


Kushoto ni Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Shinyanga Zuhura Waziri akimshukuru Meneja Mahusiano wa mgodi wa Williamson Diamonds Limited Joseph Kaasa kwa kukubali ombi lake kuisaidia shule ya msingi Bugweto yenye changamoto lukuki ikiwemo madarasa yaliyochakaa yakiwa yametawaliwa na nyufa na chini kuna vumbi (hakuna sakafu).

Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Shinyanga Zuhura Waziri akimshukuru Meneja Mahusiano wa mgodi wa Williamson Diamonds Limited Joseph Kaasa kwa msaada wa madawati 25 katika shule ya Bugweto
Kulia ni Meneja Mahusiano wa mgodi wa Williamson Diamonds Limited Joseph Kaasa akizungumza baada ya kukabidhi madawati hayo,ambapo alisema wamekuwa wakisaidia na wataendelea kusaidia jamii katika masuala mbalimbali ya kijamii
 
 Kijana akiwa amebeba moja ya madawati hayo
Zoezi la Kupakia madawati kutoka shule ya msingi Mwadui iliyopo katika mgodi wa Williamson Diamonds Limited uliopo katika wilaya ya Kishapu kwenda shule ya msingi Bugweto iliyopo katika wilaya ya Shinyanga likiendelea
Hapa ni katika shule ya msingi Bugweto- Wa pili kutoka kulia ni Meneja Mahusiano msaidizi wa mgodi wa Williamson Diamonds Limited Gamba Isaac Mtoni akieleza jambo baada ya kufika katika shule hiyo.Wa kwanza kulia ni mwalimu mkuu msaidizi katika shule hiyo Suzana Mabula.
Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Shinyanga Zuhura Waziri (CCM) na diwani wa kata ya Ibadakuli Msabila Mabula
Meneja Mahusiano msaidizi wa mgodi wa Williamson Diamonds Limited Gamba Isaac Mtoni akieleza kuhusu msaada wa madawati walioutoa kwa shule hiyo ili kupunguza changamoto ya madawati katika shule hiyo.
Meneja Mahusiano msaidizi wa mgodi wa Williamson Diamonds Limited Gamba Isaac Mtoni akishikana mkono mwalimu mkuu msaidizi katika shule hiyo Suzana Mabula
Hili ni darasa katika shule ya msingi Bugweto,linatumika kama ofisi ya walimu,halina meza wala viti vya walimu. Pichani ni walimu wa shule hiyo wakiendelea na kazi
Shule hii pamoja na kuwa na changamoto lukuki ikiwemo madarasa mabovu,uhaba wa matundu ya vyoo pia haina hata Bendera ya taifa

Wanafunzi wakiwa darasani katika shule ya msingi Bugweto iliyopo katika manispaa ya Shinyanga. Darasa limechakaa

Shule ipo mjini Shinyanga-Hili ni moja ya madarasa katika shule ya msingi Bugweto iliyopo katika manispaa ya Shinyanga.Kuta zina nyufa chini hakuna sakafu kuna vumbi na mawe na wanafunzi wanaendelea na masomo kama kawaida
Mwalimu katika shule ya msingi Bugweto akiendelea kufundisha
Meneja Mahusiano msaidizi wa mgodi wa Williamson Diamonds Limited Gamba Isaac Mtoni akitoka kuangalia nyumba ya mwalimu mkuu wa shule ya Bugweto,ambayo hata hivyo haitumiwi na mwalimu mkuu kutokana na ubovu wake.Inaelezwa kuwa shule hiyo haina nyumba za walimu matokeo yake walimu wanaishi nje ya eneo la shule

Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Bwana Kadama Malunde akiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Bugweto iliyopo katika manispaa ya Shinyanga.

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post