Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limefuta mkutano wa hadhara wa Chadema uliopangwa kufanyika katika Uwanja wa Miembe Saba mjini Chalinze.
Mkutano huo uliokuwa ufanyike jana, ulikuwa uhutubiwe na Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa kamati ya Chadema, Frederick Sumaye.
Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Pwani Baraka Mwago alisema
jana kuwa alishangazwa na hatua hiyo ya ghafla ya polisi kwa kuwa
mkutano huo ulifuata taratibu zote na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chalinze,
aliruhusu kufanyika kuanzia saa 6.00 mchana hadi saa 12.00 jioni.
Alisema
wakati maandalizi yote yakiwa tayari, ilipotimia saa nane mchana
waliitwa polisi na kuelezwa kuwa mkutano huo umezuia kwa maelezo kuwa
intelijensia ya polisi imeonyesha kuwa ungehudhuriwa na viongozi wengi
wa kitaifa, hivyo polisi Chalinze haijajipanga kutoa ulinzi kwa viongozi
hao.
“Hii sababu imetushangaza kwa sababu kiongozi wa kitaifa ambaye angehudhuria ni Sumaye peke yake."
Kwa
mujibu wa Katiba ya Chadema kipengele cha 7.5.3 (f) inamtambua mjumbe
wa kamati kuu au baraza kuu anayeishi katika mkoa kuwa ni mjumbe wa
baraza la mkoa husika.
“Kutokana
na kipengele hicho, Sumaye ana sifa za kuhudhuria mkutano huu kwa
sababu anaishi Kiluvya wilayani Kisarawe,” alisema Mwagu.
Alisema
lengo la mkutano huo, lilikuwa ni kuutambulisha uongozi mpya wa Chadema
kwa wananchi baada ya kufanyika uchaguzi mdogo Juni 4, mwaka huu
wilayani Mkuranga.
Katibu
wa Chadema mkoani humo, Halfani Milambo alisema waliandika barua
kuwataarifu polisi na likakubali, lakini walishangazwa kuzuiwa baada ya
kufika katika Uwanja wa Miembe Saba walikotakiwa kufanya mkutano.
“Tuliwaandikia
barua tarehe Agosti 4 na siku iliyofuata Agosti 5 tulikubaliwa na Mkuu
wa Polisi Chalinze (OCD), SSP J. Magomi kufanya mkutano kwa masharti,” alisema.
Alitaja
masharti ambayo jeshi hilo liliwapa kuwa ni pamoja na kutokuwapo kwa
maandamano ya bodaboda, ya miguu au magari, kutokukashifu chama au
utawala wa kiongozi yeyote na kuzingatia muda wa kuanza na kumaliza
mkutano.
Alisema
kuwa cha kushangaza jana baada ya kukamilisha maandalizi yote ikiwamo
kufanya matangazo na kufunga vyombo vya muziki, baadhi ya viongozi
waliitwa kwenye Ofisi ya Polisi Wilaya ya Chalinze na kuambiwa wasifanye
mkutano huo.
Alisema
walielezwa kuwa ujumbe ambao unaenea kwenye mtandao unasema mkutano huo
utaleta watu wengi sana, hivyo usalama utakuwa mdogo.
Kamanda
wa Polisi mkoani Pwani, Boniventura Mushongi alisema lengo la Polisi si
kuwakataza kufanya mkutano, lakini kilichoonekana ni kuwa walikiuka
maelekezo kwani awali walipaswa kufanya mkutano wa ndani na si wa nje.
“Sisi
hatuwakatazi kufanya mikutano yao, lakini ni vema wafuate makubaliano,
maana sisi Jeshi la Polisi tuliwaruhusu wafanye mkutano wa ndani lakini
tulishangazwa kuona wanaanza kufanya nje huku wakipiga muziki,” alisema.
Mushongi
alisema pia polisi inazuia mikutano yote ambayo haina madiwani wala
wabunge katika eneo husika, jambo ambalo halikuwa kwenye maelekezo ya
OCD.
“Chadema
katika eneo la Chalinze hawana diwani wala mbunge, hivyo wamekosa sifa
za kufanya mkutano huu. Kama ni kikao cha ndani hatuna tatizo wafanye
hata wakialika watu 200,” alisema Mushongi.
Hata hivyo, Mushongi alisema Chadema Pwani walipopeleka barua ya maombi mkutano huo walipewa masharti hayo.
Mbowe: Tuko tayari kwa lolote
Wakati
hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema yeye na
makamanda wake wako tayari kwa lolote kwa ajili ya kutetea misingi
thabiti ya utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
Akizungumza
jana, Mbowe alisema hakuna mtu wa kuwafundisha makamanda wa Chadema,
hivyo mikutano ya Ukuta itafanyika nchi nzima kuanzia Septemba Mosi.
“Ambao
hawako tayari warudi nyuma, hakuna aliyelazimishwa, watuache sisi
tutangulie wa kufa wafe na wa kupona wapone. Haiwezekani mtu apuuze
sheria, avunje katiba halafu taifa linyamaze,” alisema.
“Sisi
tumeamua kuchukua mzigo huo kwa niaba ya wananchi wote. Kama ataua
wacha aue tu, kama atatufunga wacha atufunge tu lakini tutakuwa tumeacha
legacy (kumbukumbu) duniani,” alisisitiza.
Mbowe
alisema sifa ya kiongozi bora anayeheshimu misingi ya kidemokrasia ni
kuheshimu utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
Kwa
mujibu wa Mbowe, Rais anakiuka Katiba na sheria za nchi zinazoruhusu
vyama vya siasa kuendesha mikutano ya hadhara na hakuna mtu ndani ya CCM
anayezungumzia hilo.
Mbowe
alisema Rais amejisahau kuwa yeye (Mbowe) ni mwenyekiti wa taifa kama
alivyo Rais, hivyo anastahili kuzunguka nchi nzima kujenga uhai wa
chama.
“Rais
anazunguka kwenye mikoa anavisema vyama vya upinzani na kutoa amri
mbalimbali lakini sisi (upinzani) hatuna jukwaa la kujibu au kutoa
ufafanuzi. Anasema tusubiri hadi 2020,” alilalamika Mbowe.
“Rais
anatoa amri, wakuu wake wa mikoa wanatoa amri, wakuu wa wilaya wanatoa
amri, watu wanafukuzwa kazi ovyo. Nchi haiwezi kwenda kwa staili hii,” alisema.
“Wewe
unanyanyuka tu na kusema watu wahamie Dodoma kivipi? Issue ya kuhamia
Dodoma ni suala la kitaifa siyo mamlaka ya mtu mmoja tu kwa kuwa ni
Rais.”
“Hata Nyerere 1973 alipopitisha hoja ya watu kuhamia Dodoma kilikuwa ni kikao cha NEC ya Tanu. Mpaka leo hakuna sheria ya kuhamia Dodoma na nchi hii inaoongozwa kwa sheria.”
Mbowe alisema kwa kutambua kuwa hakuna sheria ya kuhamia Dodoma, ndiyo maana Ilani ya CCM (2015-2020) imeeleza kutengeneza sheria ya kuhamia makao makuu Dodoma.
“Hata Nyerere 1973 alipopitisha hoja ya watu kuhamia Dodoma kilikuwa ni kikao cha NEC ya Tanu. Mpaka leo hakuna sheria ya kuhamia Dodoma na nchi hii inaoongozwa kwa sheria.”
Mbowe alisema kwa kutambua kuwa hakuna sheria ya kuhamia Dodoma, ndiyo maana Ilani ya CCM (2015-2020) imeeleza kutengeneza sheria ya kuhamia makao makuu Dodoma.
“Hakuna
sheria. Rais hawezi kuamua matakwa yake binafsi yakawa ni sheria ya
nchi. Alipaswa apeleke muswada wa sheria bungeni na ipitishwe na Bunge
siyo kauli ya mtu mmoja,” alisisitiza Mbowe.
Lissu: Tutafuata sheria
Wakati
huohuo, mwanasheria Mkuu wa Chadema na mbunge wa Singida Mashariki,
Tundu Lissu amesema katika utekelezaji wa Ukuta watafuata sheria kwa
kupeleka barua za taarifa ya mikutano kwa wakuu wa polisi nchi nzima saa
48, kabla ya kuanza mikutano hiyo Septemba Mosi mwaka huu.
Akizungumza
juzi katika mahojiano na Redio ya Sauti ya Ujerumani (DW), Lissu
alisema mikutano hiyo itafanywa kwa kufuata sheria na taratibu ikiwamo
kutoa taarifa kwa wakuu wa polisi wa wilaya.
Lissu
ambaye aliachiwa na mahakama juzi kwa dhamana, alitoa kauli hiyo baada
ya kuulizwa kwanini chama chake kisitafute njia mbadala ya operesheni
Ukuta ambayo Serikali imesema itakabiliana nayo kwa njia yoyote ile.
“Tumesema
hatutafanya mkutano wowote usiokuwa na taarifa.Tutapeleka taarifa kwa
wakuu wa polisi wilaya wote Tanzania nzima kama inavyotakiwa. Sasa hiyo
hatuvunji sheria, tunatekeleza sheria,” alisema Lissu.
Mbunge
huyo, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi na kuidharau
mahakama, alibainisha kuwa mikutano ya hadhara kuanzia Septemba Mosi,
itafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi kama Katiba ya nchi na sheria ya
vyama vya siasa inavyoeleza.
Alisema
sheria inasema chama cha siasa ambacho kimeandikishwa kikitaka kufanya
mkutano wowote wa hadhara wa siasa, kinatakiwa kupeleka barua ya taarifa
kwa mkuu wa polisi wa wilaya saa 48 kabla ya mkutano huo.
“Sheria inasema huyo ambaye tunampelekea taarifa atupe ulinzi kwenye mikutano yetu. Ndicho tunachotaka,” alisema Lissu.
Alipoulizwa
kama ni sawa iwapo polisi ikisema haiwezi kuwapa ulinzi na wasifanye
mkutano katika eneo husika kwa wakati huo, Lissu alijibu, “(OCD) Ana
uwezo wa kutuambia msifanye leo, msifanye kwenye eneo hili au msifanye
saa hii, lakini hana uwezo wa kukataa katakata.”
Mbunge huyo alisema kilichotokea nchini na kinachofanyika sasa si mikutano kudhibitiwa bali inakatazwa.
Mbunge huyo alisema kilichotokea nchini na kinachofanyika sasa si mikutano kudhibitiwa bali inakatazwa.
“Hakuna sheria inayokataza au inayowapa mamlaka ya kukataza mikutano moja kwa moja kama hakuna tangazo la hali ya hatari,” alisema Lissu.
Alisema kama Magufuli hataki mikutano atangazie dunia kwamba Tanzania ina hali ya hatari.
“Akitangaza hali ya hatari tutamwelewa na wengine tutamuuliza kilichotokea ni kitu gani mpaka kuwe na hali ya hatari,” alisema Lissu.