Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 07 Agosti, 2016 ametembelea Msikiti na Makanisa yaliyopo Chato
Mjini Mkoani Geita na kuendelea kuwasihi Watanzania kuombea amani na
utulivu katika nchi bila kujali tofauti za dini, makabila na kanda
wanazotoka.
Rais Magufuli ametoa ujumbe huo mara baada ya kusali ibada ya
Jumapili katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato, na
baadaye kutembelea Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Stephano Parokia ya
Chato, Kanisa la African Inland Church la Chato na kumalizia katika
Msikiti wa Omar Bin -L-Khattab wa Chato.
Dkt. Magufuli amesema pamoja na Watanzania wote kuungana kuombea
amani na utulivu pia hawana budi kutekeleza kwa vitendo Maandiko
Matakatifu ya Biblia yasemayo "Asiyefanya kazi na asile" kwa kuhakikisha
kila mmoja anachapakazi kwa juhudi na maarifa ili kuharakisha maendeleo
ya Taifa.
"Ndugu zangu nawashukuru sana, muendelee kuliombea taifa
hili, taifa letu ni la umoja, sisi wote ni Watanzania, tuendelee
kumuomba mola wetu, kudumisha amani yetu, kujenga umoja wetu kwa dini
zote, makabila yote na vyama vyote, kwa sababu mola wetu anatupenda sisi
sote" Amesema Rais Magufuli.
Aidha, mara baada ya kuwasalimu waumini wa Kanisa Katoliki la Bikira
Maria Parokia ya Chato, Rais Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia
ujenzi wa jengo jipya la Kanisa hilo ambapo amefanikiwa kukusanya
Shilingi Milioni moja za papo kwa papo.
Tayari Dkt. Magufuli alishachangia ujenzi huo kwa kutoa Shilingi
Milioni kumi tarehe 03 Aprili, 2016 na ametoa wito kwa watu mbalimbali
kujitokeza kuchangia ujenzi wa Kanisa hilo.
Katika Msikiti wa Omar Bin-L-Khattab na Makanisa ya Anglikana na
African Inland Church Rais Magufuli amechangia Shilingi Milioni tano kwa
kila moja kwa ajili kuendeleza na kukarabati majengo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Chato