RAIS
John Magufuli ametoa ubani wa Sh milioni 10 kwa familia za askari wanne
waliouawa katika shambulio la ujambazi Mbande wilayani Temeke mkoani
Dar es Salaaam, huku akiwataka askari kutokuvunjika moyo katika utendaji
wao wa kazi kutokana na mauaji ya wenzao, bali walitumie kama kigezo
cha kufanya kazi kwa bidii.
Aidha,
Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi,
Inspekta Jenerali Ernest Mangu na wanafamilia wa askari wote waliopoteza
maisha.
Askari
watatu kati ya wanne waliofariki katika shambulio hilo la Jumanne usiku
katika eneo la benki ya CRDB Mbande, Dar es Salaam ambalo watu wenye
silaha waliwavamia wakiwa kazini na kuwaua na kupora bunduki mbili aina
ya SMG na risasi 60, waliagwa jana katika Viwanja vya Polisi Barabara ya
Kilwa.
Akizungumza
wakati wa kuaga miili hiyo katika shughuli iliyoongozwa na Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, IGP Mangu alisema baada ya
tukio hilo kutokea, aliwasiliana na Rais Magufuli ambaye alionesha
kusikitishwa sana na tukio hilo na kumpa pole yeye, askari pamoja na
familia za marehemu.
Miili
ya askari walioagwa jana ni Koplo Yahaya Malima aliyesafirishwa kwenda
kuzikwa kijiji cha Kibuta, wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Tito Mapunda
aliyesafirishwa kwenda kijiji cha Migoli, wilaya ya Iringa Vijijini
mkoani Iringa na Gaston Lupanga aliyesafirishwa kwenda mjini Songea
mkoani Ruvuma kwa maziko.
Askari
mwingine Koplo Khatib Ame Pandu alisafirishwa Jumatano jioni kwenda
kwao Zanzibar ambako maziko yalifanyika siku hiyo hiyo usiku.
Viongozi
mbalimbali wa serikali walipata fursa ya kutoa salamu za rambirambi
katika msiba huo, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
aliamuru wale wote waliofanya uhalifu huo pamoja na wale wanaofanya
vitendo vya uhalifu jijini Dar es Salaam kushughulikiwa ipasavyo.
“Katika
hili ninaomba wale wa haki za binadamu wanisamehe, kitendo hiki si cha
kuvumilika hata kidogo kwa kuona wale ambao wamekula kiapo kutulinda
sisi, leo sisi tunakwenda kuwaua wao halafu tunyamaze, mimi nasema hapa
hadharani …Afande Sirro twanga tu yeyote mtakayekutana naye msituni,” alisema Makonda.
Makonda
alisema kazi ya amani ya vyombo vya ulinzi ni kubwa hivyo ipo haja ya
kuangaliwa upya kwa taratibu na sheria kuona ni namna gani askari kama
hao wanaopoteza maisha wakiwa bado vijana wadogo kuwajengea hata nyumba
ili kuwapa faraja wale wanaowaacha nyuma yao.
Naye
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi
Simon Sirro alisema kitendo walichofanya wahalifu hao kuua askari ni
sawa na kuwasha moto hivyo na wao watajibu mapigo na kuhakikisha
wahalifu hao wanapatikana.
“Wameuwasha
moto na sisi tutauwasha moto kwelikweli na katika hili tutaomba watu wa
Tume za Haki za Binadamu kutosimama upande wowote,” alisema Sirro.
Aidha,
Waziri Mwigulu aliagiza Jeshi la Polisi kuendelea bila kukoma kuwasaka
majambazi na wahalifu wote na kuhakikisha wanakamata waliofanya tukio
hilo.
Mwigulu
pia ameagiza viongozi wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wizara
yake kuangalia upya sheria na kuona namna bora ya kuwasaidia askari kuwa
na bima za maisha, huku akiwataka kuhakikisha wanaharakisha mafao kwa
familia za marehemu yanaandaliwa mapema.
“Mara
nyingi kumekuwa na tabia ya usumbufu kwa ndugu na jamaa za wafiwa
kusumbuliwa na maandalizi ya mirathi kuchukua muda mrefu na wakati
mwingine tukio kama hili tumeshuhudia wote lilivyotokea na askari wetu
kufa wakiwa kazini lakini bado itaundwa tume kuchunguza ili mafao
yalipwe kwa wafiwa,” alisema Mwigulu.
Naye
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema kitendo cha
kushambulia askari na kuwaua ni kuichokoza mamlaka ya nchi na kulaani
wote walioshabikia mauaji hayo kwa namna yeyote ile.
“Kitendo
hiki si cha kushabikia na tuache kabisa kushabikia vitendo vya uvunjifu
wa sheria, lakini pia tutambue kuwa sheria au Katiba ya Nchi haina
mjadala,” alieleza Masaju.
Mwenyekiti
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Nyanduga
alilaani na kupinga mauaji ya kikatili na kusema kuwa ni kinyume cha
haki za binadamu na haki ya kuishi ya kila mtu ipo ndani ya Katiba.
Mbali
na Mwigulu, viongozi wengine wa serikali waliotoa heshima za mwisho kwa
miili ya marehemu ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harison Mwakyembe,
Masaju, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest
Rwegasira.
Pia
IGP Mangu, Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, Meya wa
Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)
Biswalo Mganga, Mkuu wa Makosa ya Jinai, DCI, Diwani Athuman pamoja na
makamishna mbalimbali wa Polisi, mahakimu na wanasheria.
Katika
hatua nyingine, mmoja wa majeruhi katika tukio hilo, Said Ally (36)
aliyelazwa katika Hospitali ya Temeke, amefanyiwa upasuaji na kutolewa
risasi aliyopigwa.
Ally
ambaye ni mfanyabiashara katika eneo la Mbande Magengeni karibu na
benki ya CRDB ambako tukio hilo lilitokea, alijeruhiwa kwa risasi hiyo
wakati alipotoka nje ya duka lake kuangalia kuna nini baada ya kusikia
milio ya risasi.
Akizungumzia
hali ya Ally, Ofisa Habari wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alisema
kwa mujibu wa taarifa alizopewa na madaktari ni kwamba majeruhi huyo
alifanyiwa upasuaji huo jana.
“Taarifa
nilizopewa ni kwamba amefanyiwa upasuaji leo (jana) na ametolewa risasi
ambayo ilikuwa mguuni kwake pamoja na ganda la risasi, lakini
anaendelea vizuri,” alisema Msumba.
Majeruhi
mwingine ni Azizi Ally aliyekuwa akiuza chipsi katika mgahawa jirani na
benki hiyo, alijeruhiwa na risasi mkono wake wa kushoto wakati
akikimbia kuokoa uhai wake.
Azizi
ambaye alishonwa nyuzi sita katika mkono huo, alisema anaendelea vizuri
kwa kuwa alipata matibabu muda mfupi baada ya tukio hilo na aliruhusiwa
kurejea nyumbani.
Social Plugin