RAIS John Magufuli amesema kwamba binadamu wanapaswa kuwa wamoja hata kama wana tofauti mbalimbali zikiwamo za kimadhehebu ya dini, siasa na kanda, huku akiwaomba viongozi wa dini kuendeleza juhudi zao za kuliombea taifa na kuwaunganisha wananchi licha ya tofauti walizo nazo.
Dk Magufuli alitoa kauli hiyo jana baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu ya kuadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya Ndoa ya Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na mkewe, Anna iliyofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam jana.
Hafla ya Jubilei hiyo ilifanyika nyakati za mchana kwenye Ukumbi wa Kardinali Rugambwa, uliopo kando ya Kanisa la Mtakatifu Petro-Oysterbay na ilitanguliwa na Misa ya shukrani, iliyofanyika katika kanisa hilo majira ya asubuhi.
Jubilei hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais Magufuli na mkewe, Mama Janeth , Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa Awamu ya Sita wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume, Mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, mawaziri wakuu wastaafu Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba na Edward Lowassa.
Misa Takatifu ya Shukrani iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Askofu Josephat Lebulu na kuhudhuriwa na maaskofu na maaskofu wakuu saba, akiwemo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu, Rais Magufuli alimpongeza Rais mstaafu Mkapa kwa kutimiza miaka 50 ya ndoa na alieleza kuwa ndoa hiyo iliyowaunganisha wanandoa wanaotoka katika madhehebu tofauti ya Kikristo, imetoa fundisho kubwa kuwa binadamu wanapaswa kuwa wamoja, hata kama wana tofauti mbalimbali zikiwemo za kimadhehebu ya dini, siasa na kanda.
Rais Magufuli alisema miaka 50 ya ndoa ya Mkapa ambaye ni muumini wa Kanisa Katoliki na mkewe, Anna ambaye ni muumini wa Kanisa la Kilutheri, inawafundisha Watanzania wote hususan wanasiasa kuishi kwa upendo na kuilinda amani waliyonayo.
Alitoa mwito kwa viongozi wa dini kuendeleza juhudi zao za kuliombea taifa na kuwaunganisha wananchi licha ya tofauti walizo nazo.
Kwa upande wake, Rais mstaafu Mkapa pamoja na kuwashukuru viongozi wote, ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria Misa ya Shukrani na Jubilei hiyo ya miaka 50 ya ndoa yake, alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia ndoa yake umri mrefu.
Aidha, alitoa mwito kwa Watanzania kupenda na kushirikiana huku akibainisha mafunzo aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa dini kuwa “Kila mmoja ni zawadi kwa mwenzake.”
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alimpongeza Rais mstaafu Mkapa na mkewe, Mama Anna kwa kuadhimisha miaka 50 ya ndoa na amewasihi Watanzania kuiga mfano mwema uliooneshwa na wanandoa hao ambao wamedumu katika imani bila kuyumba.
Kardinali Pengo alisema ndoa ya Rais mstaafu Mkapa inaifundisha jamii kuwa tunaweza kuishi kwa imani zetu bila kubadili dini.