Rais Magufuli -"Nitoe Wito Kwa Walimu Tanzania Nzima, Mnatafuta Matatizo,Msijaribu Kula Hela ya Serikali"

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji hapa nchini kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya fedha hizo.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 01 Agosti, 2016 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha wananchi wa Katoro na Buseresere Mkoani Geita.

Katika agizo hilo Dkt. Magufuli amewaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa lengo la kupata mgao mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.

"Ninafahamu mgao wa fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa katika shule zao, ili kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi waliopo, wanafunzi kama wapo laki nne yeye anasema shule yangu hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi hela zikija za wanafunzi laki tano, za wanafunzi laki moja wagawane.

"Napenda nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta matatizo, msijaribu kula hela ya Serikali" Amesema Rais Magufuli.

Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli pia ametaka viongozi wa ngazi zote katika Mikoa kuhakikisha wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule zote zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa kuanzia sasa ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.

"Na nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tarafa, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, kila mmoja awe na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki kutoa hela ambayo haitakiwi" Amesisitiza Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ambaye ametumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania Mpya pia amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea wananchi wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.

Aidha, Dkt. Magufuli amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri nyingi za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu huo kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika Halmashauri husika.

"Hivi kwa nini Halmashauri msingekuwa na maafisa wenu wazuri na mkawa na mashine za kielektroni kwa ajili ya kukusanya fedha? Amehoji Dkt. Magufuli na kuongeza kuwa;

"Tena mawakala wengine ndio hao hao wamekuwa wakikusanya kodi hata kwa wananchi wanyonge wenye vibiashara vidogo vya kuuza mchicha bila hata kuwaonea huruma"

Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemaliza ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita na yupo nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato

01 Agosti, 2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post