WAKATI takribani asilimia 20 ya viongozi wa umma kwa mwaka 2011 hadi mwaka jana hawakuwasilisha matamko ya mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa wakati, mwaka huu serikali imetangaza kuhakiki matamko ya mali za viongozi 500.
Aidha, serikali hiyo imebainisha wazi kuwa haitowafumbia macho viongozi, watakaoshindwa kuwasilisha matamko ya mali zao kwa mujibu wa sheria, ikiwemo viongozi watakaowasilisha matamko ya mali yatakayobainika kuwa na udanganyifu.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki wakati akifungua warsha ya wadau, kujadili taarifa ya matokeo ya utafiti kuhusu hali ya maadili nchini Dar es Salaam jana.
Kairuki alikiri kuwa hata katika tafiti nyingine ndogo, zilizofanyika kuhusu hali ya maadili nchini pamoja na takwimu kubadilikabadilika, lakini zilibainisha kuwepo kwa viongozi wasiowasilisha matamko yao ya mali na wengine kutowasilisha kwa wakati.
Alisema taarifa hiyo ya utafiti kuhusu hali ya maadili ya viongozi nchini kwa miaka mitano kuanzia 2011 hadi mwaka jana, ilibainisha kuwa pamoja na kuwepo kwa mwamko wa viongozi kuhusu suala zima la maadili, bado asilimia 20 ya viongozi hao wa umma hawakuwasilisha matamko yao ya mali kwa wakati.
“Tumepokea taarifa hii na imetutia hamasa kwa kweli, tumeona asilimia 20 hawarejeshi kwa wakati matamko yao, hawa ni wengi sana ikizingatiwa kuwa ni viongozi, tunatoa onyo hakuna atakayefumbiwa macho endapo atakiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kwani atachukuliwa hatua stahiki za kisheria,” alisisitiza.
Alisema kwa kawaida endapo kiongozi asipowasilisha tamko la mali zake hadi ifikapo Desemba 31, huhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, lakini pia inapothibitika kuwa alikiuka kwa makusudi sheria hiyo ya maadili ya viongozi huchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema mwaka huu, kuna jumla ya viongozi wa umma 15,624 kati ya hao viongozi 500 tayari wameshatengewa fedha kwa ajili ya mali zao kuhakikiwa na endapo fedha zitapatikana idadi hiyo inaweza kuongezeka na kufikia 1,000.
“Miaka ya nyuma tulikuwa tunahakiki kwa mwaka viongozi 100 hadi 200, safari hii tumejipanga kuanza na viongozi 500. Lakini katika hili tunaomba wananchi nao watusaidie kuhakiki mali za viongozi hawa wa umma kwani sheria inawa ruhusu kufanya hivyo, ili kuweza kubaini viongozi wadanganyifu,” alisema.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Kessy aliyefanya utafiti huo kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, alisema lengo la utafiti huo ni kuangalia hali halisi ya maadili nchini kuanzia viongozi hadi kwa wananchi.
Social Plugin