Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kulifungia kwa miezi 36
gazeti la “MSETO”. Amri ya kulifungia Gazeti hilo imetolewa kwa Tangazo
la Serikali Na. 242 lililotolewa tarehe 10 Agosti, 2016. Uamuzi huo
umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 Sura ya 229,
kifungu 25(1).
Kifungu hicho kinasema “Waziri
akiona kwamba kwa ajili ya manufaa ya umma au kwa ajili ya kudumisha
amani na usalama inafaa afanye hivyo aweza kutoa amri na kuitangaza
kwenye Gazeti la Serikali ambayo itaeleza kwamba gazeti lililotajwa
katika amri hiyo litakoma kutolewa tangu siku (ambayo katika fungu hili
itaitwa ''tarehe ya kuanza kutumika'') itakayotajwa katika amri hiyo”
Uamuzi
huo unazuia gazeti la Mseto kuchapishwa katika njia nyingine yoyote
ikiwa ni pamoja na mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya
Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta Sura ya 306.
Aidha,
hatua hii ya kulifungia gazeti hilo imechukuliwa baada ya Msajili wa
Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda mrefu kuanzia Septemba, 2012 hadi
Agosti, 2016 kumtaka Mhariri wa gazeti kuacha kuandika habari za
upotoshaji, uchochezi na za uongo na zisizo zingatia maadili ya taaluma
ya uandishi wa habari bila mafanikio.
Kutokana
na hali hiyo, Serikali kwa masikitiko makubwa, imelazimika kuchukua
uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo wa kuandika
na kuchapisha habari ya uongo na kughushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali
za Serikali kwa nia ya kumchafua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wa Serikali kwa lengo
kutaka kumchonganisha na wananchi ambao wamekuwa na matarajio makubwa
kwa uongozi wa Awamu ya Tano.
Pamoja
na makosa mengine, hivi karibuni gazeti lao katika toleo Na. 480 la
tarehe 4 hadi 10 Agosti, 2016 lilichapisha na kusambaza makala na barua
ya kugushi kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yenye kichwa cha
habari kisemacho “Waziri Amchafua JPM” Amhusisha na rushwa ya uchaguzi
mkuu, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano.
Kwa
mujibu wa vyombo vya uchunguzi vya Serikali, imebainika kwamba nyaraka
hiyo imeghushiwa na wahariri na walipotakiwa kuleta uthibitisho wa
nyaraka waliyotumia katika gazeti lao, walishindwa kuleta vithibitisho
hivyo
Ninatoa
wito kwa wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari
kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari
ambayo ukizingatiwa hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha Serikali
inasisitiza kwamba inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia
maadili, weledi na Sheria za nchi na kwamba Serikali itaendelea
kushirikiana navyo.
Serikali
ya Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayoanisha
uhuru na mipaka ya habari kama vile Tamko la Kimataifa la haki za
Binadamu la mwaka 1948, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na
Kisiasa, na Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu na Watu 1981.
Mikataba
na matamko hayo kwa pamoja licha ya kuanisha uhuru wa habari ambao
Tanzania imeruhusu kwa kiwango kikubwa pia, imeweka ukomo wa uhuru huo
kwa kukataza habari za uongo, uzushi na uchochezi.
Ninapenda
kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kujenga uhusiano mzuri na wa
kirafiki kati yake na wadau wa sekta ya habari. Aidha ninasisitiza tena
wadau wa sekta hii kuzingatia Sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya
uandishi wa habari ili kujenga heshima ya tasnia ya habari na kulinda
amani ya nchi yetu.
Mhe. Nape M. Nnauye (Mb,)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
Social Plugin