Katibu Mkuu wa chama cha ADA-TADEA nchini John Shibuda ameibuka na kumkingia kifua rais John Pombe Magufuli na kudai kuwa wanaosema ni dikteta wamekosa ubunifu mpya wa kutengua mvuto wa siasa,sera na utumishi wa awamu ya tano na kuvitaka vyama vya upinzani kuachana na siasa za mipasho na vijembe visivyotatua kero za umaskini,ujinga na uchumi wa kaya. Mwandishi wa Malunde1 blog,Kadama Malunde anaripoti.
Shibuda ambaye alikuwa mbunge wa Maswa Magharibi kwa tiketi ya Chadema na CCM kwa vipindi tofauti kabla ya kuhamia ADA-TADEA,alitoa kauli hiyo juzi mjini Shinyanga wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alivinyoshea vidole vyama vyenzake vya upinzani na kuvitaka kubadilika na kuwa na vikosi kazi imara vya kubuni tiba mbadala na bora ya kutengua utumishi wa rais Magufuli.
“Naomba wapinzani tusiwe vifuniko vya madhira dhulumati ya maovu dhidi ya ustawi wa utawala bora wa awamu ya tano kwani rais Magufuli ni kizibuo cha maovu na ni tanuru la kukaushia mitaji ya malighafi ya siasa za ukweli bandia ulionogeshwa na utamu unono wa maneno ya uongo ya kufanana na ukweli”,alieleza Shibuda.
Katibu huyo mkuu wa ADA TADEA aliwataka watanzania na wanasiasa waliopevuka kuwa na matamshi yaliyoshiba lishe ya mawazo makini ya kunufaisha fikra za watanzania na washirika wa kimataifa wa Tanzania.
“Kwa kuwa ukweli haurogeki,mahimizo ya rais Magufuli siyo udikteta bali ni hamira ya kuibua msisimuko wa uhuru na maendeleo ,na uhuru ni kazi na asiyekula asinufaike na bofulo la wavuja jasho wa Tanzania”,alieleza.
“Rais Magufuli ni katili sana kwa maovu ya kudhulumu ustawi na maendeleo ya jamii na taifa na ,ninawaomba watanzania wampongeze kwa kuwa katili kwa maovu..na kama ni katili basi na dini zote duniani ni katili kwa sababu dini zote duniani ni katili kwa maovu ya dhambi zinazodhulumu waja wa mwenyezi mungu na watumishi wa mungu siku zote wamekuwa wakihamasisha uadilifu ambao utatupeleka peponi”,aliongeza Shibuda.
Alisema rais Magufuli ni katili wa maovu na rafiki wa uadilifu hivyo atapongezwa na wapenda uadilifu na atakwazwa na wapenda uovu kwa hali hiyo ni juu yake achague kupendwa na waadilifu ili awe na safari ya kwenda peponi au achague kupendezesha waovu waliojipanga kwenda jehanamu.
“Lazima tukubali kuwa rais Magufuli kakausha tabia zembe za uwajibikaji wa serikali,amekuwa tanuru la kukaushia uhalifu wa ufisadi na kwamba msisimuko wa jamii unaoshangilia zomea zomea dhidi ya serikali kupitia vijembe vya vyama vya upinzani ajenda hizo zimenyauka”,alisema.
“Taifa limepata rais mwenye utumishi changamfu wa kugusa hisia za jamii, kwa hiyo sasa vyama vya siasa tusitafute mifereji ya kutorokea mkauko,mnyauko na msinyao wa ajenda zenye virutubisho vya kugusa hisia za jamii na kukonga mioyo ya wananchi ”,aliongeza Shibuda.
Alivitaka vyama vya upinzani viwe na ubunifu mpya wa kutengua mvuto wa siasa,sera na utumishi wa awamu ya tano wa rais Magufuli,viachane na na siasa za mipasho na vijembe visivyotatua kero za umaskini,ujinga,uchumi wa kaya na wapinzani wawe na vikosi kazi vya kubuni tiba mbadala na bora ya kutengua utumishi wa rais Magufuli.
“Natoa wito kwa vyama vya upinzani kwamba vyama vya upinzani vijipange upya,viwe na mtazamo mpya wa utendaji huduma za kisiasa,duniani pana mabadiliko ya mazingira ya tabia nchi,hali ya hewa ya nchi mbalimbali kwa hiyo sasa Tanzania ya awamu ya tano ni dunia ya mabadiliko ya mila,jadi na utamaduni wa utendaji wa dira ya siasa za kukabiliana na ukosoaji wa utumishi wa awamu ya tano”,alifafanua.
Aidha alisema Tanzania ina mfumo wa vya vingi visivyopungua 21,hakuna chama chochote cha siasa Tanzania ambacho kipo kwa maslahi ya kukweza chama kingine kwa kila chama kipo kugombania kushika hisia za jamii na kushika madaraka ya dola.
“Kila chama cha kisiasa kina uhuru wa kuwa na tafsiri binafsi ya kuhusu mfumo wa utumishi wa serikali na utumishi wa siasa wa chama tawala kwa hiyo hakuna chama ambacho kinalazimishwa kufungumana na tafsiri ya chama chochote kingine zaidi ya kufungamana na siasa,sera na itikadi ya chama chenyewe”,alisema.
Alisema vyama vinaweza kuwa na ushirikiano wenye dhamira sahihi unaoendana na dhamira ya kukuzwa na kukwezwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla ndiyo maana chama ADA-TADEA kina ushirikiano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Msikilize hapa Mheshimiwa John Shibuda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu rais Magufuli na vyama vya siasa nchini Tanzania.