Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Taarifa Kamili Kuhusu Kaburi la Mtoto Albino Kufukuliwa Shinyanga...Diwani Acharuka, Kamanda wa Polisi Afunguka


Wananchi,viongozi wakifukua kaburi la mtoto mwenye ualbino katika kijiji cha Bunambiyu wilayani Kishapu


Katika hali isiyokuwa ya kawaida kaburi alilozikwa  mtoto mwenye ualbino Michael Juma mwenye umri  wa miaka miwili  na nusu limefukuliwa  na mwili wake kutolewa kasha kuzikwa tena baada ya kuibuka utata uliohusisha imani za kishirikina kwamba baadhi ya viungo vya mwili wa mtoto huo havipo baada ya kukatwa.Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog Kadama Malunde,anaripoti.


Mtoto huyo mkazi wa kijiji cha Bunambiyu kata ya Bunambiyu wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga alifariki siku ya Jumamosi Agosti 13,2016 kisha kuzikwa siku ya Jumapili wiki iliyopita Agosti 14,mwaka huu na mwili wake ulifukuliwa siku ya Alhamis Agosti 18 mwaka huu.

Baada ya mazishi ya mtoto huo taarifa zilianza kusambaa kuwa viungo vingine vya mwili havipo hali iliyosababisha kufukuliwa na kufanyiwa uchunguzi mwili wake kisha kuzikwa tena.

Kaburi  hilo  lilifukuliwa baada ya jeshi la polisi kufika katika kijiji cha Bunambiyu wilaya ya Kishapu nyumbani kwao marehemu wakiwa wameambatana na viongozi  wa Chama cha Albino mkoa wa Shinyanga.


Baada ya  jeshi la polisi kufika eneo la tukio walizungumza na familia husika wananchi na viongozi wa kijiji hicho juu ya kuwepo utata wa mwili wa marehemu jambo ambalo walilipinga vikali.

Akitoa maelezo ya kufukua mwili huo, afisa upelelezi wa polisi wa wilaya  ya Kishapu Meshack Sumuni kuliibuka mvutano  mkubwa huku baadhi ya viongozi wa eneo hilo na wananchi  waliojitokeza wakionyesha kutokukubaliana na hatua ya kufukua kaburi hilo kwa madai kuwa marehemu amekufa kifo cha kawaida na alizikwa na viungo  vyake vyote vya mwili.

“Ndugu  zangu wananchi  tumekuja hapa kujiridhisha baada ya kupata taarifa  ya  utata uliojitokeza na tumepata  kibali cha mahakama cha kufukuwa kaburi hilo  na haya ni maelekezo kutoka ngazi za juu, nawaomba mtupe ushirikiano  hata mimi sina wasiwasi  na hiki kifo, hatupendi  kumsumbua marehemu ila tunahitaji majibu ya mwisho”,alisema Sumuni.

Akizungumza  kabla  ya  kufukua mwili  huo  katibu  wa chama cha watu  wenye  ualbino  mkoa  wa  Shinyanga  Lazaro  Anael  alisema kitendo  cha kufukua kaburi  kinaleta  mpasuko kwa jamii na hisia tofauti, kwa kuwa wao  ndiyo  walioshiriki  kwenye  mazishi  kwani wanaweza kuogopa kuzika pindi anapofariki mtu mwenye ualbino.

Alisema marehemu alizikwa akiwa na viungo vyake vyote  vya  mwili na wazazi ,viongozi  wa kijiji na kata walijiridhisha kwa kuuona mwili na hakuna kiungo kilichokatwa.

Akifafanua zaidi Anael alisema cha kushangaza baada ya mazishi alipigiwa simu na mkurugenzi wa shirika la Under The Same Sun  Vick  Ntetema akimueleza  kuwa kaburi linatakiwa kufukuliwa kwa madai kuwa kuna utata umejitokeza.

Kutokana  na hali hiyo Nael alisema hali hiyo  ilimshtua kwani Vick Ntetema alikuwepo siku ya mazishi na alishuhudia na kuona hakuna kiungo  cha mwili kilichokatwa  kisha kukubaliana  kufanya  mazishi, huku  akibainisha  kuwa  mazishi yalizingatia taratibu zote  za mila na desturi na hawakuwa na shaka yoyote kwa kuwa kila kitu kilikuwa wazi.

Naye  mzazi wa marehemu  Juma  Masudi  alisema marehemu baada ya kuugua walimpeleka kituo cha afya Bunambiyu ambako alipatiwa matibabu na kurudishwa nyumbani lakini ilipofika siku ya Jumamosi hali ilibadilika na akafariki saa tatu usiku na kesho yake yalifanyika mazishi.

“Kabla ya mazishi siku ya Jumapili Agosti  14 mwaka huu ndugu wote na viongozi wa kijiji tulimuona marehemu alikuwa na viungo vyote vya mwili na hakuna kilichokatwa kwa vile leo polisi wamefika wasema kuna utata umejitokeza mimi niko tayari wafukuwe ili wajiridhishe kama viungo vyote vipo”,alisema Masudi.

Naye  mwenyekiti wa kijiji cha Bunambiyu Jonathan  Katela alisema taratibu zote za mazishi zilifuatwa na hakukuwa na tatizo lolote lililojitokeza  na wananchi walishiriki kwenye mazishi huku akishangazwa na utata ulioibuka na kusababisha kaburi hilo kufukuliwa ili kuchunguza mwili wa marehemu.

Awali kabla ya kufukua mwili huo ,diwani wa kata  ya Bunambiyu  Richard Sangisangi  aliyekuwa eneo la tukio alisema hayuko tayari kushiriki katika zoezi hilo la ufukua kaburi ili kujiridhisha  wakati marehemu alikufa kifo cha kawaida na viungo vyake vya mwili vilikuwepo  wakati  anazikwa na kushangazwa na utata uliojitokeza huku akihoji unatoka wapi.

Alisema suala hilo ni la kuzungumza na kufikia muafaka siyo mpaka kufukua kaburi kwani hali hiyo ni kuendelea kuipa uchungu familia ya marehemu kwa kuwakumbusha nyuma,huku akiitaka serikali kuwa inashiriki kwenye mazishi ya watu albino pindi wanapofariki ili kuondoa utata kama huo.

“Kitendo hiki ni kumsumbua marehemu ambaye ameshapumzika...siwezi kuchuma dhambi kufukua mwili wa marehemu... hivi kweli ni nani mwenye uchungu zaidi kuliko wazazi wa mtoto huyu  ,mpaka wanataka tufukue kaburi mimi kama diwani nasema siko tayari kushiriki na ninaondoka nyie endeleeni na polisi waliokuja hapa’’,alisema diwani  huyo huku akiondoka eneo la tukio.

Akizungumza baada ya zoezi la kufukua mwili wa marehemu kisha kukagua upya mwili huo lililoshuhudiwa na wananchi,askari na viongozi wa kijiji,daktari Helena Kaunda kutoka kituo cha afya Bunambiyu alisema viungo vyote vya mwili viko sawa na hakuna kilichokatwa.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi mkoa wa  Shinyanga Muliro   Jumanne  Muliro alithibitisha kaburi hilo kufukuliwa  kwa lengo la kujiridhisha ili kuondoa utata na uvumi ulioenezwa kuwa  huenda  mtoto huyo aliuawa ili wakate viungo vyake na ndiyo maana  hatua hiyo ikachukuliwa ili kumaliza mashaka yaliyojitokeza.


Alisema baada ya kutokea kifo cha mtoto huyo jeshi la polisi lilifanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa ni kifo cha kawaida kama vinavyotokea kwa binadamu wengine wasio na ualbino hivyo kuruhusu mwili huo uzikwe lakini cha kushangaza baada ya mazishi ndiyo kukaibuka uzushi kuwa pengine mtoto huyo aliuawa.


“Ili  kupata  majibu ya uvumi huo niliagiza vitu vyote muhimu vya uchunguzi  vinavyoweza  kutoa  majibu sahihi vifanyike ,tuliongea na wanafamilia ya marehemu na ndugu wa marehemu walikubali ingawa wengi walikataa  tukafanya  zoezi hilo na sasa mashaka hayo yatakuwa yamekwisha baada ya kukuta hakuna kiungo kilichokatwa vyote vipo.


Kamanda Muliro alieleza kuwa  uvumi huo na mashaka unahusisha baadhi ya taasisi zinazojihusisha  na masuala ya ualbino ambazo hata  hivyo hakuzitaja ,hali ambayo ilitokana na mtoto huyo kuvimba mwili na kutoka damu puani  hali ambayo inaweza kuwa iliwatia mashaka na kuzusha maneno.


Hata hivyo alisema kutokana na vifo vya watu wenye ulemavu wa ngozi kuhusishwa na imani za kishirikina  huenda ndiyo maana uliibuka uvumi hasa kutokana na kwamba marehemu alikuwa anatoka damu puani kabla ya kifo chake.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog 
Bofya Hapa Kuangalia Picha 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com