MAMLAKA ya Udhibiti wa Mawasiliano hapa Nchini (TCRA) imewaonya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaojisajili katika mitandao hiyo kwa kutumia majina na taarifa za uongo.
James Kilaba Kaimu Mkurugenzi wa TCRA amesema, vitendo vya watu kujisajili katika mitandao ya kijamii kwa kutumia majina na taarifa zisizo sahihi, ni kosa kisheria na kwamba wanaofanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kilaba ameyasema hayo jana, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuongeza ufahamu kuhusu matumizi sahihi na salama ya mitandao ambayo inasimamiwa na Kitengo cha dharura cha kuitikia matukio ya usalama kwenye mitandao hapa nchini (TZ-CERT).
“Tumeamua kuzindua kampeni hii ili kuwasaidia wananchi kuepuka makosa ya kimtandao na kuepuka kufanyiwa utapeli au wizi mitandaoni kwa sababu matukio mengi ambayo yamekuwa yakiripotiwa au kulalamikiwa yanazuilika kwa watu kupewa elimu ya matumizi sahihi ya mitandao,” alisema Kilaba.
Kampeni hiyo ya kuongeza ufahamu kuhusu matumizi sahihi na salama ya mitandao, itafanyika kupitia matangazo ya redio, televisheni, magazeti pamoja na mitandao ya kijamii ambapo katika mitandao ya kijamii itajulikana kama, “Darasa mtandao”.
“Miongoni mwa mambo ambayo tutawafundisha wananchi ni kutoweka wazi taarifa zao binafsi zote katika mitandao, kubadili na kutunza neon la siri (password), kutojibu ujumbe unaosema umeshinda bahati nasibu na mengineyo mengi,” alisisitiza Kilaba.