Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu (pichani) ambaye leo amefikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam na kupandishwa kizimbani dhidi ya mashtaka matatu ikiwamo kuidharau mahakama na kusababisha chuki kwa watanzania dhidi ya Rais John Magufuli na serikali yake ameachiwa kwa dhamana.
Lissu alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka matatu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Cyprian Mkeha, katika kesi iliyoanza saa 9.26 mchana hadi saa 2.25 usiku.
Hakimu alitupilia mbali kiapo cha Jamhuri kwa kuwa hakikuonesha tarehe iliyotolewa.
Kisha Hakimu akamtaka mshtakiwa kujidhamini mwenyewe kwa kusaini hati ya dhamana ya shilingi milioni 10.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi, akisaidiana na Wakili Serikali Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi,Mawakili wa Serikali Simon Wankyo na Paul Kadushi.
Kadushi alidai kuwa Agost 2,2016 akiwa na nia ya kujenga chuki dhidi ya Rais Dk John Magufuli kwamba ni dikteta uchwara.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la kwanza mshtakiwa akiwa na nia ya kuleta dharau katika mfumo wa mahakama nchini alitamka kwam a "Kesi ya kipuuzi na mashtaka yamekaa kimagufuligufuli "alinukuliwa mshtakiwa.
Shitaka la tatu linadai kuwa siku na eneo la tukio la kwanza mshtakiwa baada ya kutoka kusikiliza kesi zake mbili tofauti zinazomkabili katika mahakama hiyo akiwa na lengo la kudharau mahakama alitamka "Siwezi kufungwa mashtaka yenyewe ya kipuuzi yamekaa kimagufuligufuli" alinukuu Kadushi.
Lissu alidai kuwa maneno anayodaiwa kuyatamka katika hati ya mashtaka ni ya kweli lakini siyo ya uchochezi hivyo alikana mashtaka hayo.
Hata hivyo Nchimbi alidai kuwa upande waJamhuri unapinga dhamana dhidi ya mshtakiwa kupitia hati ya kiapo iliyowasilishwa na Mkuu wa upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala ( RCO) kwamba mshtakiwa akipewa dhamana atarudia kufanya makosa hayo kinyume cha sheria.
Pia Nchimbi aliwasilisha pingamizi la kumkataa wakili kiongozi wa utetezi Peter Kibatala kwamba ametoa maelezo polisi na kwamba anatarajiwa kuwa shahidi wa Jamhuri dhidi ya mshtakiwa.
kuhusu uwakili Kibatala alidai kuwa hakuna sheria inayomzuia kumtetea mteja wake na kwamba ni njama za upande wa Jamhuri kwa kuwa wanamhofia.
Kutokana na pingamizi la dhamana, Lissu alilazimika kujibu hoja mwenyewe baada ya upande wa Jamhuri kusisitiza kwamba Kibatala haruhusiwi kumtetea mshtakiwa hadi mahakama itakapoamua vinginevyo.
Alidai kuwa hoja za Jamhuri hazina mashiko ya kuzuia dhamana yake kwa kuwa hajatiwa hatiani na kwamba chini ya kifungu cha 148 kidogo cha (5)a hakijaanisha sababu zilizotolewa na Jamhuri kuzuia dhamana yake.
Na Mwene Saidi wa Globu ya Jamii
Social Plugin